The Last Royal Treasure: Filamu ya kuchangamsha wikiendi yako
- Ni filamu inayoongoza kwa kutazamwa katika filamu za Kikorea zilizotoka 2022.
- Kisa chake kinahusu kundi la maharamia wanaoongozwa na mwanamke.
- Kundi hili linajikuta katika vita ya kugombania shehena ya mali za kifalme na viongozi wakubwa wa jeshi.
Dar es salaam. Filamu ya ‘The Last Royal Treasure’, inahusu kundi moja la maharamia au kwa Kiingereza wanafahamika kama pirates.
Meli yao imebeba watu ambao wana historia tofauti za kimaisha. Wengine walikuwa majenerali wa vita, watoto wa manahodha, huku wengine wakiwa ni wezi walioshindikana.
Kinachovutia ni kuwa kundi hilo lenye zaidi ya watu 30, lina mwanamke mmoja tu, ambaye ndiye kiongozi wao na siyo mwingine bali kapteni Hae Rang.
Mwanadada huyu ni mrembo kweli kweli na ukikutana naye kwa mara ya kwanza huwezi kujua kuwa ngumi yake moja inatosha kukukutanisha na malaika mtoa roho.
Hata hivyo, maisha ya kundi hili yanabadilika baada ya kuwakamata Wajapani waliokuwa wakivua samaki kwenye eneo la Jeoson ikizingatiwa kuwa, katika kipindi hicho Japan na Joseon walikuwa na uadui.
Wakati wakipanga adhabu ya kuwapatia Wajapan, aidha kifo au kuwatosa katikati ya bahari, mtoto mmoja aliyekuwa na Wajapan hao akaropoka.
“Hapana jamani msituue, hatuajaja kuiba samaki wenu ila…” “ilaaa…” kundi zima likaitikia kwa hamu ya kutaka kujua neno lililofuata.
“Tumekuja kutafuta mali za kifalme zilizopotea,” alimalizia mtoto huyo.
“Mali?” kundi zima likashangaa kwa kutazamana, Wajapani wakashusha vichwa chini, mtoto kashamwaga mtama kwenye kundi la kuku wenye njaa.
Hae rang ambaye ni kiongozi wa kundi hilo, anatoa amri ya kuanza kuisaka shehena iliyopotea ambayo imejaa mali za kifalme. Picha| Butwhythopodcast.
Kumbe kuna shehena ya kifalme iliyojaa dhahabu, fedha na vito vya thamani, ambayo iliibiwa miaka ya nyuma na haijulikani ilipelekwa wapi.
Shehena hiyo ukiipata kwa kipindi hiki, unaweza kuhama kwa Bi Nyau unakoishi hadi kuitwa ukae meza moja na wakina Elon Musk, Mark Zuckerberg na Jeff Bezos. Fahamu kuwa, katika kiwango hicho, kina Baharesa na Mwamedi watakuwa wakikutazama kwa mbaali.
Basi, maharamia hawa hawakutaka kuremba, hapo hapo kapteni Hae Rang anaamuru kundi hilo kunyanyua nanga na safari inaanza kutafuta shehena hiyo.
Utajiri unaoleta vita
Harakati za kutafuta shehena ya kifalme inazua mambo. Kumbe kuna watu wengine nao wanaitafuta shehena hiyo.
Umesikia wapi mali zikatafutwa na mtu mmoja tu? Napozungumzia watu wengine simaanishi watu wa kawaida bali ni viongozi wa jeshi wenye vyeo vya maana.
Wanapofanikiwa kuvuka vikwazo vya hapa na pale hatimaye kundi la Hae Rang linalipata pango ambalo shehena za kifalme zimefichwa.
Wanachokiona hata wao hawaamini. Pango lenye ukubwa wa kiwanja cha mpira limejaa mabox yaliyojazwa kila aina ya madini.
Kwa furaha wanakumbatiana na kuruka ruka, lakini ghafla unasikika mlipo kutoka nje ya pango hilo. Wakiwa wanajiuliza ni nini kinaendelea kundi la jenerali wa vita Bu Heung Soo linaingia kwenye pango hilo.
Haya sasa fahari wawili kwenye zizi moja. Vita inayofuata hapo sio ya kusimuliwa maana hakuna anaekubali kugawana wala kumuachia mwenzie mali hizo.
Unahisi ni nani ataondoka na utajiri huo?, je ni timu Hae Rang au Bu Heung? Majibu yapo kwenye filamu ya The Last Royal Treasureambayo utaipata kwenye jukwaa la filamu la Netflix.
Kwenye filamu hii utakuna na mastaa wengi wa filamu za Kikorea, akiwemo mwanadada Han hyo Joon aliyefanya vizuri kwenye filamu nyingi ikiwemo Happiness na Sword Fraternity.