Uzalishaji saruji wapaa kwa miaka sita mfululizo
- Wafikia tani milioni 6.53 mwaka 2021.
- Uzalishaji wa saruji kuendelea kupaa huku bei ikipanda.
- Mahitaji ya nyumba yachangia kuongeza uzalishaji.
Dar es Salaam. Uzalishaji wa saruji nchini Tanzania umepaa kwa miaka sita mfululizo iliyopita hadi kufikia tani milioni 6.53 mwaka 2021, huku wataalam wa ujenzi wakisema kuongezeka kwa shughuli za ujenzi kumechangia ongezeko la uzalishaji huo.
Saruji ni bidhaa muhimu katika ujenzi ambapo kuna zaidi ya aina 15 za saruji duniani. Hata hivyo, Saruji ya kawaida ya Portland (OPC) ndiyo aina ya saruji inayotumiwa na kuzalishwa kwa wingi Tanzania na ulimwenguni kote.
Ripoti ya takwimu za “High Frequency Data” za Mei 2022 zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hivi karibuni inaeleza kuwa uzalishaji wa saruji wa mwaka jana umeongezeka kwa asilimia 16.5 kutoka tani milioni 5.60 zilizozalishwa mwaka 2020.
Hilo ni sawa na ongezeko la tani 925,468 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Hata hivyo, ongezeko hilo siyo la bahati mbaya kwa sababu kwa miaka sita iliyopita uzalishaji wa saruji umekuwa ukiongezeka kila mwaka tangu mwaka 2016.
Mathalan, mwaka 2015 uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu ya ujenzi ulikuwa tani milioni 3.14 lakini ukapanda hadi tani milioni 4.04 mwaka uliofuata kabla haujapanda zaidi hadi kufikia tani milioni 6.53 mwaka jana.
Huenda uzalishaji huo ukaendelea kupaa zaidi kwa mwaka 2022, kutokana na ripoti hiyo ya NBS kueleza kuwa uzalishaji wa robo ya kwanza ya mwaka huu (January hadi Machi) ulikuwa tani milioni 1.73 ambao umeongezeka kutoka tani milioni 1.46 kipindi kama hicho mwaka 2021.
Pia zalishaji huo ni wa juu zaidi kuwahi kurekodiwa kwa miaka sita iliyopita kwa mwaka unaoishia Machi.
Kwa sasa, bei ya saruji katika baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam ikiwemo Bunju inauzwa kati ya Sh15,000 hadi Sh16,000 kwa mfuko wa kilo 50.

Sababu kuongezeka kwa uzalishaji
Baadhi ya wataalam wa ujenzi wanasema ongezeko hilo la uzalishaji wa saruji nchini limechangiwa na kuongezeka kwa shughuli za ujenzi wa nyumba za kuishi, biashara na miundombinu ya usafirishaji.
“Saruji ni bidhaa muhimu na ya lazima katika ujenzi wowote nyumba au miundombinu, kadiri watu wanavyojenga basi wanahitaji saruji zaidi,” anasema Rachel Essau, mtaalam wa ujenzi na mipango miji.
Essau anaeleza kuwa ongezeko la watu hasa katika miji inayokuwa kwa kasi ikiwemo Dar es Salaam inaongeza mahitaji ya nyumba na watu wanakuwa hawana chaguo lingine zaidi ya kununua saruji kama moja ya malighafi za ujenzi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2016 kuhusu mikopo ya ujenzi wa nyumba inaeleza kuwa mahitaji ya nyumba nchini yanakadiriwa kufikia nyumba 200,000 kila mwaka ambapo mpaka sasa kuna upungufu wa nyumba 3 milioni za makazi ya watu.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Waziri Dk Ashatu Kijaji katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2022/23 alisema licha ya uzalishaji wa saruji kuongezeka bado bei ya bidhaa hiyo inapanda.
Alisema Machi 2021, bidhaa hiyo iliuzwa kwa wastani wa Sh17,662 na Machi mwaka huu iliuzwa kwa wastani wa Sh18,283 sawa na ongezeko la Sh621 kwenye kila mfuko wa saruji wa kilo 50.
Hata hivyo, alisema katika hotuba hiyo kuwa Serikali inachukua hatua kudhibiti upandaji holela wa bei ya bidhaa hiyo ili kuwapunguzia wananchi ukali wa maisha kwa sababu karibu bei za bidhaa zote zimepanda.
Tanzania ina viwanda 14 vya saruji ambavyo vinamilikiwa na kampouni mbalimbali ikiwemo Huaxin Tanzania, kampuni tanzu ya Huaxin Cement Ltd, kampuni ya Saruji ya Ngamia, wakati Lake Cement Ltd na Kisarawe Cement Ltd.
Habari hii imeandikwa na Lucy Samson na Daniel Samson.
Latest
