Nane Nane 2024: Fursa lukuki wakulima kujinoa kiteknolojia

August 3, 2024 3:16 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Maonesho hayo yanatoa fursa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kuonyesha kujifunza teknolojia mbalimbali za kuongeza tija. 

Arusha. Maonesho ya kimataifa ya kilimo maarufu Nane Nane yameendelea kuzinduliwa katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania ikiwa ni moja ya fursa adimu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kuonesha bidhaa zao na kujifunza teknolojia mbalimbali za kuongeza tija kwenye uzalishaji. 

Maonesho hayo hufanyika kila mwaka kati ya wiki ya mwisho ya mwezi Julai na wiki ya kwanza ya Mwezi Agosti huku kilele kikiwa ni Agosti 8 ambapo wakulima na wadau wengine wa kilimo hupata fursa ya kuonesha bidhaa na huduma wanazotoa ili kufungua fursa za masoko na kujifunza mbinu nyingine za kuzalisha mazao yao.  

Katika maonesho yaliyozinduliwa rasmi leo jijini Arusha kwa ajili ya Kanda ya Kaskazini, miongoni mwa bidhaa na huduma zinazovutia na kuelimisha wengi ni zile za teknolojia zinazosaidia kazi na kuongeza ufanisi.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amewataka viongozi wa mikoa ya kanda hiyo kuhamasisha wakulima, wafugaji na wavuvi kuyatumia maonesho hayo kujinoa kiteknoklojia.

Maonesho hayo yanayofanyika jijini Arusha katika viwanja vya Themi- Njiro yakivutia maelfu ya watu kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Tanga na Kilimanjaro.

“Niwaombe viongozi mtumie fursa hii kuwaleta wakulima wafugaji na wavuvi kutoka maeneo yetu kwa wingi ili wapate fursa ya kujifunza teknolojia na kwenda kuzitumia ili kukuza uchumi,” amesema Babu wakati akifungua maonesho hayo Agosti 3,2024.

Miongoni mwa bidhaa za kiteknolojia zilizonogesha maonesho ya Nane nane kwa mwaka 2024 kwa Kanda ya Kaskazini ni mashine ya kupukuchua na kupepeta aina tisa ya mazao na nyingine ya kuchakata chakula cha mifugo zilizotengenezwa na kampuni ya Imara Teknology. 

James Prosper, mtaalamu wa kilimo wa Imara Teknology ameiambia Nukta Habari kuwa mashine hizo ni msaada mkubwa kwa wakulima na wafugaji wenye mashamba na mifugo mingi.

Mashine yachakata gunia 80 kwa saa nne

‘Mashine hizi zinaweza kufanya kazi kwa masaa manne mfululizo, ina maana mkulima anaweza kuchakata (kupukuchua na kupepeta) gunia 80 mpaka 100 ndani ya saa nne, na mfugaji anaweza kuchakata hadi tani moja.

…Zikipumzishwa kwa saa moja mkulima au mfugaji anaweza kuendelea kuchakata mazao mengi zaidi,” amesema Prosper.

Mashine hizo zinauzwa Sh 1.6 milioni hadi Sh1.9 milioni huku zikihitaji utaalamu wa kuziendesha pamoja na kiasi cha dizeli au petroli cha lita moja hadi tatu kwa siku jambo ambalo linaweza kuwasaidia wakulima wenye kipato na viwango vikubwa vya mazao kurahisisha uchakataji wa mazao yao. 

Miongoni mwa mashine zinazosaidia kuchakata mazao ndani ya muda mfupi ikiwemo kupukuchukua na kupepeta takriban gunia 100 kwa saa nne. Picha|Lucy Samson/Nukta.

Miongoni mwa mashine zinazosaidia kuchakata mazao ndani ya muda mfupi ikiwemo kupukuchukua na kupepeta takriban gunia 100 kwa saa nne. Picha|Lucy Samson/Nukta.

Hata hivyo, baadhi ya wakulima na wafugaji wenye kipato kidogo huenda mashine hizo zikawa ghali kiasi cha kuwafanya kushindwa kumudu licha ya umuhimu wa teknolojia katika kuongeza tija.

Teknolojia nyingine iliyovutia macho ya wahudhuriaji wengi katika maonesho haya ni ‘Screen house’ inayohusisha kulima ndani ya eneo moja lililofunikwa kwa neti na karatasi ngumu ili kuzuia jua, upepo na wadudu waharibifu wa mazao.

Uwekezaji wa aina hiyo ya kilimo unahitaji Sh12 milioni na unaweza kulima kwa muda wa zaidi ya miaka 10 huku mkulima akitakiwa kulima mazao ya mboga mboga ambayo soko lake lipo juu zikiwemo Pilipili Hoho za rangi ‘sweet watermelon’ na matango.

Enable Notifications OK No thanks