Mambo ya kuzingatia unapotumia VPN Tanzania

September 11, 2024 6:35 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuzingatia sheria na kanuni za matumizi ya VPN zinazozuia usambazaji wa maudhui yaliyokatazwa ikiwemo picha za ngono.

 Dar es Salaam. Matumizi ya Mtandao Binafsi (VPN) yanaendelea kukua kila uchwao na ni sehemu ya maisha ya baadhi ya watumiaji wa huduma ya mtandao duniani kote ikiwemo nchini Tanzania.

Kwa baadhi ya huduma, VPN ni takwa la lazima kutokana na sera zao za kulinda faragha za watumiaji huku baadhi ya taasisi au watu hutumia VPN ili kuongeza ubora wa huduma zao, kupata huduma ambazo hazipatikani katika eneo hilo kwa wakati huo au kujilinda dhidi ya wadukuaji wa mtandaoni.

Jarida la Forbes la Marekani limebainisha kuwa mpaka mwaka 2024 kuna jumla ya watumiaji bilioni 1.6 wa VPN duniani ambapo zaidi ya asilimia 70 hutumia kwa ajili ya ulinzi wa data zao.

Licha ya kuwa hakuna takwimu rasmi za watumiaji wa VPN nchini Tanzania ni ukweli uliowazi kuwa wapo wanaotumia huduma hiyo na hilo linathibitika mara baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA Oktoba 13, 2023, kuwataka watumiaji wa huduma hiyo kusajili aina ya VPN wanazotumia.

Hivyo tunaweza kusema matumizi ya VPN nchini Tanzania si haramu ila ni lazima isajiliwe kwanza kwa TCRA kwa kutoa taarifa zote muhimu ikiwemo anuani ya itifaki ya mtandao yaani (IP Address).

Pamoja na uamuzi huo wa TCRA kutoungwa mkono na baadhi ya Watanzania mamlaka hiyo ilishikilia msimamo wake na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kudhibiti upatikanaji na usambazaji wa maudhui yaliyokatazwa.

VPN inavyofanya kazi

Jukumu la kwanza la VPN huwa ni kubadili anuani ya itifaki mtandao (IP Adress) na kumruhusu mtumiaji kutengeneza msimbo (itifaki bandia) anayotaka kutambulika nayo kwa wakati huo.

Baada ya hapo mtumiaji anaweza kupata huduma anayotaka kwa kutumia anuani mtandao ya bandia ambapo ukomo wa upatikanaji wa huduma hizo hutegemeana na uwezo wa VPN yake.

Mathalani hivi karibuni watumiaji wa mtandao wa Telegram nchini Tanzania hawawezi kuutumia mtandao huo pasi na kuwasha VPN maana yake wanatumia itifaki bandia ili kupata huduma ya mtandao huo.

Kutokana na ukweli kwamba matumizi ya VPN hayazuiliki hususan katika upatikanaji wa huduma muhimu ikiwemo mawasiliano Nukta Habari imeandaa dondoo za kuzingatia kabla hujachagua VPN ya kutumia kwa kurejea maoni na mapendekezo ya wahariri wa jarida la masuala ya sayansi na teknolojia la Marekani la CNET.

  1. Kasi ya intaneti

Moja ya mambo muhimu kuzingatia wakati wa kuchagua VPN ni kasi ya intaneti kwa kuwa VPN zinaweza kupunguza au kuongeza kasi ya intaneti kwa sababu zinapitisha data kupitia seva iliyosimbwa kabla ya kuwasiliana na programu, tovuti na huduma zingine za intaneti badala ya muunganisho wa moja kwa moja. 

Kwa matumizi yanayohitaji kiasi kikubwa cha data kama vile michezo ya video ya mubashara (live streaming games), kuangalia video zenye mng’ao angavu kuanzia 4K unahitaji VPN isiyopunguza kasi ya intaneti kwa chini ya asilimia 25 ambapo kiwango cha kawaida cha kupungua huwa ni asilimia 50.

Kwa mujibu wa CNET ExpressVPN inatajwa kuwa mtandao binafsi rahisi na wenye kazi ingawa itakulazimu kulipia kiasi cha Sh35,300 kwa mwezi mmoja, Sh27,223 kwa mwezi kwa bili ya miezi 6 mfululizo na Sh217,920 kwa mwaka.

Mwonekano wa ukurasa wa ExpressVPN ikionesha vifaa tofauti vilivyounganishwa na huduma hiyo. Picha |ExpressVPN

  1. Usalama na faragha

Kigezo kingine muhimu kuzingatiwa ni usalama wa faragha, VPN huficha anuani ya mtumiaji ambayo inaweza kufichua taarifa zako za kijiografia. Inashauriwa  kuchagua VPN yenye usimbaji fiche wa 256-bit, pia ambao miongoni mwa sera zake ni kutoacha kumbukumbu za mtumiaji.

Pia, ni vyema kuchagua VPN yenye kipengele cha ‘kill switch’, ambacho kinawafaa sana watumiaji wanaohitaji usiri mkubwa kama waandishi wa habari za uchunguzi.

Baadhi ya VPN huwa na njia mbili za ulinzi ili kuhakikisha kuwa taarifa zinalindwa vizuri na kufanya iwe vigumu kwa mtoa huduma ya intaneti kujua kuwa VPN inatumika.

NordVPN ni chaguo zuri ikiwa mtumiaji anatafuta VPN yenye vipengele vingi na kasi ya juu na ina vipengele vingine kama vile ‘double VPN’, ‘Onion Over VPN’ na ‘Meshnet’ kwa usalama na faragha zaidi.

Kipengele cha ‘meshnet’ kinakuruhusu kutuma mafaili kwa usalama na watumiaji wengine wa NordVPN. Pia ina kipengele cha ‘Split Tunneling’ kinachowezesha kuchagua ni programu na tovuti zipi zitumie VPN na zipi zisitumie.

Gharama ya VPN hii ni Sh35,400 kwa mwezi mmoja, Sh163,200 kwa mwaka na Sh 221,700 kwa kipindi cha miaka miwili. Malipo hufanyika kupitia Google Pay, Amazon Pay, UnionPay, ACH Transfer na sarafu mtandao (Cryptocurrencies).

  1. Seva za VPN 

Ni muhimu kuchagua VPN yenye seva nyingi ambazo hutoa wigo mpana wa kufanya kila kitu mtumiaji anachotaka kufanya mtandaoni na kutoa ulinzi wa ziada unaohitajika.

Kadri kampuni ya VPN inavyokuwa na seva nyingi katika nchi mbalimbali, ndivyo kasi ya intaneti inavyokuwa nzuri na ndivyo mtumiaji atakavyoweza kufungua tovuti na huduma zaidi.

Baadhi ya VPN huruhusu kutuma faili kubwa kupitia seva zao zote, wakati nyingine zina seva maalum kwa ajili ya kupakua au kutuma nyaraka za mfumo huo.

Ikiwa unatafuta VPN nzuri unayoweza kutumia gharama kidogo, Surfshark ni chaguo bora. VPN hii ina sifa nyingine kama kasi, vipengele vingi muhimu, na inaweza kutumika kwenye vifaa vingi iwezekanavyo.

Vifaa tofauti vinavyoweza kuunganishwa na kutumia VPN ya Surfshark. Picha| Surfshark

Ni rahisi Kutumia na ina programu kwa vifaa maarufu kama Apple TV na Linux.

VPN hii huuzwa Sh122,600 kwa mwaka wa kwanza au Sh163,500 jumla kwa miaka miwili ya kwanza, kisha Sh163,500 kwa mwaka baada ya kipindi cha ofa kuisha, ambayo bado ni nafuu kuliko punguzo la bei za VPN nyingine kama ExpressVPN au NordVPN.

  1. Kifaa unachotumia

Unapofikiria kununua VPN ni muhimu pia kuzingatia kama inafanya kazi kwenye vifaa vyote unavyotumia aidha kompyuta, simu za mkononi na televisheni za kisasa, ikiwa inatumika kompyuta yenye mfumo wa uendeshaji wa Linux, VPN ambayo ina programu yenye picha (GUI) kama vile Surfshark, Proton, na PIA ndio inapaswa kuchaguliwa ili iwe rahisi kutumia.

Unaweza pia kuweka VPN kwenye router ili kulinda vifaa vyote vilivyounganishwa kwenye mtandao wako wa nyumbani.

Ni muhimu pia kuzingatia idadi ya vifaa vinavyoweza kutumia VPN kwa kuwa nyingi huruhusu kuweka programu hiyo kwenye vifaa vingi iwezekanavyo, lakini inaweza kuwekewa kikomo cha idadi ya vifaa nane hadi 10 ambavyo vinaweza kutumia VPN hiyo kwa wakati mmoja.

Hii ni moja wapo ya VPN bora za bila malipo zinazopatikana ingawa haina vipengele vyote vya toleo linalolipiwa, ni salama na kasi.

VPN hii hutoa vipengele vya msingi kama vile uunganishi salama na upatikanaji wa seva kutoka nchi tano. Ina kasi kubwa kwa ajili ya kazi nyingi kama vile utazamaji wa video na ni rahisi kutumiwa kwenye vifaa vyote.

Pamoja na toleo la bure lipo linalolipiwa linalotoa vipengele zaidi kama vile matumizi ya data yasiyo na kikomo, upatikanaji wa seva zaidi, na unganishaji wa pamoja kwenye vifaa vingi. 

Proton VPN inagharimu Sh27,236 kwa mwezi, Sh163,418 kwa mwaka, au Sh294,170 kwa miaka miwili (mpango wa mwaka mmoja na wa miaka miwili upya unagharimu Sh217,925 kwa mwaka).

Hata hivyo, pamoja na kuwa VPN huwezesha upatikanaji wa maudhui ambayo hayapatikani katika eneo fulani kama filamu, michezo au programu tumishi ni makosa kutumia VPN kupakua au kusambaza maudhui yaliyokatazwa.

Maudhui hayo yasiyoendana na sheria, kanuni, maadili na utamaduni wa Mtanzania ni pamoja na picha za ngono.

Kanuni ya 16(2) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta kuhusu Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020 inasema mtu hatatoa, hatamiliki au hatasambaza teknolojia, programu, programu tumizi au kitu chochote kinachoendana na ambacho kinaruhusu au kumsaidia mtumiaji kupata maudhui yaliyokatazwa.

Kwa mujibu wa TCRA utoaji, umiliki au usambazaji wa teknolojia, programu, programu tumizi au kitu chochote kinachoendana na ambacho kinaruhusu au kumsaidia mtumiaji kupata maudhui yaliyokatazwa ni kosa la jinai, linaloadhibiwa baada ya kutiwa hatiani, kwa faini ya shilingi za Kitanzania zisizopungua milioni tano au kifungo kisichopungua miezi kumi na mbili au vyote kwa pamoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks