Rais Samia awataka Mawaziri kuwajibika, wakitumia vizuri fedha za ndani

November 18, 2025 4:26 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Awasisitizia matumizi ya rasilimali kwa uadilifu, 
  • Asema huenda Tanzania ikawa imepungukiwa sifa kupata mikopo kimataifa.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amelitaka Baraza jipya la Mawaziri kuwajibika kwa Wananchi na kuhakikisha linatumia vyema rasilimali za ndani kutekeleza shughuli za maendeleo.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Novemba 18, 2025, Ikulu, Dodoma baada ya uapisho wa mawaziri wanaounda baraza hilo akisisitiza kuwa hakuna kisingizio kitakachokwamisha utekelezaji wa miradi ya Serikali kwa wakati.

“Kazi yetu kuanzia leo ni kuwajibika kwa Wananchi, kuwajibika kwa Taifa hili, kuwajibika kwa nchi yetu Tanzania,” amesema Rais Samia.

Licha ya Serikali hiyo kuahidi mambo mengi yanayotakiwa kukamilika ndani ya miaka mitano ijayo Rais Samia amesema hatasita kuwachukulia hatua mawaziri wazembe ambao hawataendana na kasi ya uongozi wake.

“Mimi sioni shida kubadilisha na mnanijua… nitabadilisha mpaka nipate yule ambaye atafanya kazi kwa moyo mkuu na kwa moyo mmoja,” ameongeza.

Fedha za ndani kugharamia shughuli za maendeleo

Kiongozi huyo wa nchi amesema kuwa awamu ya pili ya uongozi wake itatekeleza miradi ya kimkakati kwa kutumia fedha za ndani kabla ya kuhusisha washirika wa maendeleo kutokana na Tanzania kupungukiwa sifa ya kupata mikopo hiyo.

“Muhula wa pili wa Serikali ya awamu ya sita tutaanza kufanya miradi wenyewe, halafu mashirika yatatukuta njiani kisha tutakwenda nao. Tutaanza kwa fedha za ndani, kisha wakimaliza taratibu zao watatukuta tukiendelea…

…Yaliyotokea nchini kwetu yametutia doa kidogo, kwahiyo huenda yakatupunguzia sifa ya kupata hiyo mikopo kwa urahisi,” amesema Rais Samia.

Itakumbukwa kuwa kuanzia Oktoba 29, mwaka huu maeneo mbalimbali ya Tanzania yaliripoti vurugu na ghasia zilizosababisha vifo vya watu, majeruhi na uharibifu wa miundombinu, mali za umma na binafsi  zilizopelekea kusimama kwa shughuli mbalimbali nchini.

Siku chache baadae Rais Samia aliahidi kuunda tume maalumu ya kuchunguza suala hilo ili kubaini  kiini cha tatizo hilo huku akiagiza baadhi ya vijana walioshikiliwa na Jeshi la Polisi wakihusishwa na vurugu hizo kuachiliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks