Serikali ya Tanzania yaendelea kudhibiti, kuhifadhi mbegu asili kwa mustakabali wa kilimo endelevu 

April 22, 2025 6:05 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Mpango wa Benki ya Taifa ya nasaba za mimea waanza.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa imejipanga kuhakikisha mbegu na mimea ya asili zinahifadhiwa na kutunzwa kwa matumizi endelevu kwa kizazi cha sasa na cha baadae ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kulinda urithi wa kilimo nchini.

Akijibu swali la Mbunge wa viti maalum Angelina Malembeka leo Aprili 22, 2024 bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde amesema hadi sasa jumla ya sampuli 38,000 za mbegu na mimea ya asili zimekusanywa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kuziendeleza.

” Kati ya mbegu hizo sampuli 10,000 zimehifadhiwa na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA ), kupitia kitengo cha uhifadhi wa nasaba ya mimea na sampuli  28,000 zimehifadhiwa naTaasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), ameeleza Silinde.

Akiendelea kufafanua kuhusu hatua zinazochukuliwa amebainisha kuwa Serikali imeanza taratibu za kuanzisha Benki ya Taifa ya Nasaba za Mimea itakayojengwa TARI Serian, Arusha. 

Baadhi ya wageni walihudhuria leo kwenye kikao cha tisa cha mkutano wa kumi tisa wa Bunge. Picha/ Bunge Tanzania/ Istagram.

“Kwa sasa mchoro wa jengo na makadirio ya gharama za ujenzi (BOQ) vimekamilika, na hatua ya kutangaza zabuni za ujenzi inafuata,” amefafanua Silinde.

Hata hivyo, Malembeka pia ametaka kufahamu ni kwa namna gani Serikali inahakikisha mbegu hizo zinawafikia wakulima na sio kuhifadhiwa tu.

 “Serikali ina sampuli 38,000 imehifadhi hazirudishi tena kwa wakulima ili kuendeleza mzunguko wa mbegu za asili. Je Serikali haioni kuwa huo ni mpango maalumu wa kuzididimiza na kupoteza mbegu zetu za asili,” amehoji Malembeka.

Akijibu hoja hiyo, Silinde amesema kuwa ni kweli kuna baadhi ya matunda ya kisasa hayana mbegu au yakipandwa hayazai tena lakini hiyo haimaanishi kuwa mbegu asilia zinaenda kufutwa.

“Hicho ni kitu tofauti kabisa na mbegu za GMO, sasa lengo kubwa la mbegu hizi ambapo zinatumika sasa hivi ni kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi  na kukabiliana na magonjwa lakini sisi tutaendelea kusisitiza matumizi ya mbegu za asili,” amefafanua Silinde.

Katika swali la pili, Malembeka ametaka kujua mpango wa Serikali kuhusu athari za matumizi ya madawa ya viwandani kwenye mazao kama matunda.

“Kwa upande wa athari za madawa yanayotokana na kupulizia matunda Naibu Waziri ameeleza kuwa Serikali inakitengo maalumu, TPHPA  Mamlaka ya Udhibiti ya Mimea ambacho hufanya mapitio na kuangalia kiwango ambacho kinastahili kwa matumizi kulingana na viwango ambavyo vimewekwa kimataifa katika matumizi ya kemikali katika matunda ambayo yanatumika.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesisitiza dhamira ya Serikali katika kurasimisha mbegu asilia nchini kwa kusema kuwa tayari Bunge limepitisha sheria mpya ya mbegu inayoweka msingi wa kurasimisha mbegu za asili na kuziingiza sokoni. 

Waziri wa kilimo Hussein Bashe, ambaye alichangia hoja ya Naibu Waziri wa Kilimo. Picha/ NIRC.

Bashe amesema kuwa hatua ya kwanza ilikuwa kukusanya sampuli zote, na sasa TARI inaendelea kuzipanga katika makundi.

“Katika hatua ya kuanisha tayari mbegu 33 zimeshakamilika za mpunga na mahindi ambazo sasa tunaanza mchakato wa kuzitambua rasmi kwenye kanuni zetu na sheria ili ziingie madukani kama mbegu nyingine,” ameeleza Bashe.

Aidha, Bashe ameongeza kuwa wakulima watakuwa na chaguo la aina ya mbegu ikiwa watahitaji ‘traditional seed’ (mbegu asilia), OPV au ‘hybrid’ (chotara) kulingana na mahitaji yao.

Kuhusu matumizi ya viuatilifu, Waziri huyo amesisitiza kuwa TPHPA tayari imeshatambua aina 45 za viuatilifu ambavyo vinaenda kuondolewa katika orodha badala yake kuingizwa vya asili katika mchakato huo.

Serikali ya Tanzania kwa sasa imeweka msingi thabiti wa uhifadhi wa mbegu asilia huku ikiwa na mikakati ya wazi ya kuhakikisha mbegu hizo si tu zinahifadhiwa, bali pia zinafika kwa wakulima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks