Chadema: Mgogoro wa ardhi Ngorongoro hauwezi kumalizika kwa ‘mitutu’ ya polisi

August 22, 2024 4:12 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Wameitaka Serikali kurudisha haraka huduma za kijamii. 

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema mgogoro wa ardhi unaoendelea kati ya Serikali na wamasai wa Ngorongoro, Tanzania hauwezi kutatuliwa kwa kutumia nguvu za Jeshi la Polisi pekee.

Kauli ya chadema inakuja ikiwa ni siku ya tano tangu Wamasai waishio katika eneo la Ngorongoro jijini Arusha waandamane kudai haki zao za msingi kuheshimiwa na Serikali ya Tanzania huku kukiwa na madai ya polisi kutumia nguvu kuwatawanya.

Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Augusti 22, 2024 amesema matumizi ya nguvu katika kutatua mgogoro huo yanaweza kusababisha umwagaji wa damu, kuleta madhara kwa Taifa na kusababisha machafuko kusambaa katika maeneo mengine nchini.

“Serikali irudi kwenye meza ya kuzungumza na wananchi wa Ngorongoro hawa watu wana haki zote za msingi kama ni kuhamishwa wahamishwe kwa ridhaa yao, kwa ushawishi watakaopewa lakini sio kwa kutumia nguvu ya vyombo vya ulinzi na usalama,” ameeleza Mbowe.

Mbowe ameongeza kuwa chama hicho kinaungana na watu wengine wanaoamini kwamba jamii ya Wamasai wa Ngorongoro ni raia halali wa Tanzania, ambao maeneo yao ya asili yanapaswa kuheshimiwa. 

Kiongozi huyo ameeleza wasiwasi wake kuhusu amri ya Serikali kufuta vijiji, kata na vitongoji katika tarafa ya Ngorongoro akisema kuwa amri hizo zinaweza kuwanyima wananchi haki zao za msingi ikiwemo ya kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27 mwaka huu.

“Imetoka amri vya vyombo vyetu vya Serikali eti na Waziri kufuta kata, vijiji na vitongoji katika tarafa ya Ngorongoro…

…Maana yake ni kwamba kinafutwa na huduma zake zote za kijamii hawezi kupata elimu, hawezi kupata maji, hawezi wakapata afya, hawezi kujengewa barabara, hawezi kupewa chochote na Serikali yao ‘this is insane’(huu ni upuuzi),” ameelezea Mbowe.

Ikumbukwe kuwa kufuatia tangazo la Serikali Na. 673 la Agosti 2, 2024, kata 11, vijiji 25 na vitongoji 96 vya Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro vilifutwa. 

Kufutwa huko kunamaanisha kwamba wakazi wa maeneo hayo hawataweza kusajiliwa na kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Hatua hiyo imekuwa ikilalamikiwa na wadau mbalimbali wa haki za binadamu ikiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ambapo Agosti 20 mwaka huu walitaka Serikali kuheshimu haki za ardhi za jamii ya Wamaasai na kusitisha mara moja mipango ya kuwahamisha bila ridhaa yao.

“Tumeliona tangazo la Waziri mwenye dhamana Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi) likionesha kufuta baadhi ya vijiji na vitongoji vilivyopo katika eneo la Ngorongoro, nimepitia vifungu hivi na mimi kama wakili na mwanasheria hakuna kifungu chochote cha sheria kinachompa Waziri kufanya hilo alilolifanya…

… kifungu cha 30 alichokitumia ni kutafsiri kwa upotovu na ni kinyume cha sheria,” amebainisha Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Boniface Mwabukusi.

Rudisheni huduma za kijamii Ngorongoro

Mbowe ameitaka Serikali kurudisha haraka huduma za kijamii katika vijiji hivyo ili kunusuru maisha ya wananchi wa Ngorongoro huku akitoa wito kwa mamlaka husika kuhakikisha kwamba vituo vya kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura vinarejeshwa kwenye maeneo ya Ngorongoro ili wananchi waweze kutumia haki yao ya kikatiba.

“Mamlaka za uchaguzi ita tume huru ya uchaguzi ita Tamisemi ita chochote mamlaka za uchaguzi zirejeshe haraka haki ya wananchi wa Ngorongoro kushiriki michakato yote ya kuwapata viongozi kuchagua na kuchaguliwa na kuwapata viongozi wao hata kama kuna mgogoro…

…Mgogoro hauwezi kuisha kwa kuwanyima watu haki zao za msingi, haki za msingi haziwezi kuepukika kamwe kwa chochote kile,” amesisitiza Mbowe.

Mbowe pia amemuomba Rais wa Tanzania kutumia mamlaka yake kama kiongozi mkuu wa nchi kuhakikisha kwamba haki za kiraia za wananchi wa Ngorongoro zinarudishwa haraka.

“Hakuna sababu yoyote ya kuwanyima wananchi hawa haki zao za kikatiba, katiba ya nchi yetu inatoa haki ya kuishi, haki ya kusikilizwa, na haki ya kuheshimiwa,” amehitimisha Mbowe.

Enable Notifications OK No thanks