Sababu za Serikali kulivunja Jiji la Dar es Salaam

February 24, 2021 11:39 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kupunguza gharama za uendeshaji na zisizo za lazima. 
  • Halmashauri moja ya Manispaa kuteuliwa kuwa jiji. 
  • Viongozi waliojiandaa kuwa mameya wa jiji hilo wafungwa “speed governor”.

Dar es Salaam. Ili kupunguza gharama za uendeshaji na zisizo za lazima, Serikali imesema ina mpango wa kuvunja Jiji la Dar es Salaam na kuchagua manispaa moja katika jiji hilo itakayopandishwa hadhi na kuwa Jiji.

Kiutawala Jiji hilo limegawanyika katika Halmashauri sita za Serikali za mitaa: Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. 

Nyingine ni Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo na Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni.

Rais John Magufuli amedokeza jambo hilo leo Februari 24, 2021 wakati akizindua daraja la juu la Ubungo jijini humo ambalo amelipa jina la aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi aliyefariki siku chache zilizopita.

“Ninategemea kuvunja Jiji la Dar es Salaam ili tutengeneze jiji la eneo fulani tunaweza kuifanya Ilala ndio iwe jiji itategemea na namna mambo yatakavyokwenda lakini kuwa na madiwani ambao wanakaa hapa juu wanachangiwa fedha na hawana miradi ya maendeleo hili nitalikataa,” amesema Dk Magufuli akiwa juu ya daraja hilo. 

Amesema mkakati ni kuipandisha hadhi manispaa moja katika jiji la Dar es Salaam halafu zilzobaki nyingine ziwe manispaa.

“Jiji la Dar es Salaam litaendelea kuwepo lakini tutachukua eneo fulani na ninafikiri Ilala inafaa kuwa jiji maana ndio ipo katikati, Ubungo itasubiri maana barabara bado hazijatengenezwa,” amesema Rais Magufuli.


Soma zaidi: 


Kutokana na uamuzi huo, amewataka madiwani ambao walijiandaa kuwa mameya wa jiji hilo wafahamu kuwa hilo limekwisha.

“Haiwezekani unakuwa na madiwani wamekaa tu wanatengewa bajeti hizo fedha ni vizuri zikapelekwa kwenye miradi ya maendeleo ya barabara hayo ni matumizi bora ya fedha za walipakodi kwa hiyo mjiandae kisaikolojia meya atapatikana katika manispaa ya Ilala,” amesisitiza Rais.

Muonekano wa jiji la Dar es Salaam. Picha| Mtandao.

Majukumu ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliundwa na kupewa majukumu ya kuratibu na kusimamia shughuli za uendelezaji wa Jiji katika Halmashauri za Manispaa zote tano. 

Majukumu hayo ni kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Na.8 ya mwaka 1982 kifungu cha 69A ambapo majukumu yake ni pamoja na kuratibu Mamlaka na wajibu wa kila Halmashauri za Manispaa juu ya miundombinu na matumizi bora ya ardhi na uandaa Mpango Mkakati kwa ajili ya kuhakikisha kuwa panakuwepo na maendeleo endelevu ya Jiji

Kukuza ushirikiano kati ya Mamlaka za Halmashauri zote zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kuhakikisha panakuwepo amani na utulivu pamoja na kutoa msaada katika huduma kama vile Zimamaoto na maokozi, Polisi na magari ya kubeba wagonjwa na kutekeleza majukumu ya itifaki na sherehe za Kimkoa na Kitaifa.

Kwa sasa jiji hilo linamiliki vitega uchumi mbalimbali likiwemo Shirika la Uchumi la Jiji la Dar es Salaam (DDC), soko la Kariakoo, Benki ya Biashara ya Dar es Salaam (DCB), kituo kikuu cha mabasi Ubungo ambacho sasa kimeamishiwa Mbezi Luis na kimepewa jina la Magufuli.

Enable Notifications OK No thanks