Kifahamu kituo cha kwanza cha kuchaji magari ya umeme Tanzania

May 5, 2023 11:26 am · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Kituo hicho kinasimikwa mkoani Dodoma.
  • Kimejengwa na UNDP kuchagiza matumizi ya nishati safi na salama.
  • Tayari magari mawili yamenunulia kuanza kutumia kituo hicho. 

Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Programu ya Maendeleo (UNDP) Tanzania limejenga kituo cha kwanza cha kuchajia magari ya umeme (EV) jijini Dodoma, ikiwa ni hatua kubwa katika kutimiza malengo ya Taifa na kimataifa ya hali ya hewa na ukuaji wa teknolojia ya usafirishaji. 

Ujengaji huo ni sehemu ya juhudi za UNDP Tanzania kushirikiana na Serikali na wadau katika kuboresha upatikanaji wa nishati nafuu na safi, huku pia kupunguza hewa ya ukaa.

Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya UNDP Tanzania, uwekaji wa kituo cha kuchajia magari ya umeme jijini Dodoma utatoa chachu katika juhudi za nchi kuelekea katika mustakabali endelevu zaidi. 

“Tunamepokea magari mawili (ya umeme) ambayo yatakuwa Dodoma. Kupitia mradi huu wa majaribio katika makao makuu, UNDP na washarika wake wamedhamiria kuweka mshukumo ambao utachochea matumizi ya EV (magari ya umeme) katika maeneo mbalimbali ya nchi,” imeeleza UNDP katika ukurasa wake wa Twitter

Nchini Tanzania zipo taasisi na wajasiriamali waliokwisha anza safari ya utengenezaji wa magari ya umeme. Mwaka 2018 wanafunzi 14 wa Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT) waliweka rekodi ya kutengeneza gari linalotumia umeme wa betri zilizohuishwa ambazo zinatumia umemejua.

Pia mjasiriamali na mchoraji katuni maarufu nchini Masoud Kipanya tayari ameweka sokoni magari ya umeme aliyobuni mwenyewe na kutengeneza hapa nchini.

Mwezi uliopita April, 2023 Ndaki ya uhandisi na teknolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), imeonyesha hatua ya ubunifu wa magari ya umeme kwa kutengeneza gari linalochajiwa na umeme wa majumbani kwa wastani wa unit 1.8 huku likiwa na uwezo wa kutembea kilometa 90 kwa saa 1.

Sehemu ya kituo cha kuchaji magari ya umeme kilichopo jijini Dodoma. Picha | UNDP Tanzania.

Mradi wa UNDP Tanzania unalenga kuvutia matumizi ya magari ya umeme kwa kuanzisha miundombinu muhimu ili kusaidia mahitaji yanayokua ya usafirishaji endelevu katika nchini. 

“Kituo cha malipo kinawekwa kwa ushirikiano na mpango wa Nishati Endelevu kwa Wote (SEforALL), ambao unalenga kukuza ufumbuzi wa nishati endelevu duniani kote,” limeeleza shirika hilo. 

Ufungaji wa kituo cha malipo pia unatarajiwa kuunda fursa za kazi na kuvutia uwekezaji katika tasnia ya EV, ambayo itachangia ukuaji wa uchumi wa nchi. 

Mafanikio ya miradi kama hiyo katika nchi nyingine za Afrika, kama vile Afrika Kusini, Rwanda na Kenya, yanatoa mtazamo mzuri kwa soko la EV la Tanzania.

Nchini Afrika Kusini, kwa mfano, idadi ya madari ya umeme barabarani imeongezeka kwa zaidi ya asilimi 100 katika miaka miwili iliyopita, ikisukumwa na upatikanaji wa miundombinu ya malipo. 

Mradi wa UNDP Tanzania ni sehemu ya juhudi kubwa zaidi za shirika hilo katika kukuza maendeleo endelevu nchini na duniani kote.

Shirika hilo linalenga kusaidia nchi katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), ambayo ni pamoja na kupunguza utoaji wa hewa ukaa na kuendeleza suluhu za nishati endelevu.

Moja ya gari litakalotumia kituo cha kuchaji magari ya umeme jijini Dodoma kilichosimikwa na UNDP. Picha | UNDP. 

Enable Notifications OK No thanks