Wadau wa Azaki wataka ujumuishi kiteknolojia kwa walemavu

September 12, 2024 8:09 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wataka utekelezaji wa sera za walemavu na utengenezaji wa vifaa vya kiteknolojia wezeshi kwa kundi hilo.
  • Dira 2050 yatakiwa kumulika walemavu.

Arusha. Wadau wa Azaki wameitaka Serikali na watoa huduma wengine nchini kuongeza ujumuishi wa kiteknolojia kwa walemavu ili kuendana na mabadiliko ya sasa.

Wadau hao wametoa maoni hayo wakati maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yakishika kasi katika utoaji wa huduma mbalimbali huku kundi kubwa la walemavu likisahaulika na kukabiliwa na uhaba wa vifaa wezeshi.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UNWomen) Tanzania ina jumla ya walemavu milioni 3.3 huku asilimia 7.8 wakiwa ni wanawake.

Wakizunguza katika mdahalo uliohusu ujumuishi wa kiteknolojia katika wiki ya Azaki jijini Arusha leo Septemba 12, 2024 wadau hao wamesema kundi la walemavu bado lipo nyuma katika matumizi ya teknolojia hali inayowafanya kukosa taarifa na fursa muhimu.

“Unakuta mtu kaweka tangazo lake kwa njia ya picha halina maelezo sasa mtu asiyeona unakuta anakosa ile taarifa…sisi tunajitahidi kutoa elimu kwa waandishi wa habari kuwa wanapoweka video angalau waweke na maelezo ili mlemavu asiyesikia apate kuelewa,” amesema Rajab Mpilipili Mkurugenzi wa Shirika la Youth with Disability (Yodo).

Naye Doreen Kisoky kutoka kampuni ya Vodacom aliyekuwa akichangia mada katika mdahalo huo amewataka watoa huduma za kiteknolojia ikiwemo makampuni ya simu kuzingatia ujumuishi katika utengenezaji wa bidhaa ili kundi la walemavu lisisahaulike.

“Tunaongea na wakurugenzi wakuu wa kila nchi ambapo Vodacom ipo kwamba tunao wateja hawa ambao wana ulemavu…tulitoa uelewa katika nchi zote tukaibeba kama agenda kuhakikisha kwamba wanaweka bajeti kuhakikisha wanaweka huduma na bidhaa za wateja ambao ni walemavu,” amesema Kisoky.

Kisoky ameongeza kuwa kwa sasa kampuni hiyo imefundisha watoa huduma wake katika mikoa mbalimbali jinsi ya kuwasiliana na watu wenye ulemavu huku ikitengeza vifaa maalum ikiwemo simu za mkononi kwa ajili ya kundi hilo jambo linalotajwa kuongeza ujumuishi wa kiteknolojia.

Dira ya Taifa 2050 imulike walemavu

Wakati Serikali ikiendelea na maandalizi ya Dira ya Taifa ya mwaka 2050, wadau hao wameitaka Serikali kupitia dira hiyo kusimamia utekelezaji wa Sera ya Walemavu iliyopo ili kusimamia haki za kundi hilo.

“Sera zipo lakini utekelezaji wake bado…mwaka 2050 tunataka kuona utekelezaji wa hizi sera na sheria siyo zibaki kwenye makaratasi tu, tunataka ziwasaidie walemavu na kuongeza ujumuishi,” amesema Fredrick Msigallah Afisa Miradi kutoka CCBRT.

Mbali na ujumuishi wa kiteknolojia wadau hao wanatamani bajeti ya Serikali kwa walemavu iongezwe ili iweze kugharamia vifaa wezeshi kwa kundi hilo ikiwemo viti mwendo, viongeza usikivu ambavyo kwa sasa vinauzwa bei ya juu ambayo walemavu hao wanashindwa kumudu.

Aidha, Kisoky ameshauri Serikali kuandaa kanzi data itakayokuwa na taarifa za walemavu ili iwe rahisi kufikiwa na elimu, misaada kutoka kwa wadau, mashirika na taasisi zitakazoguswa kuwasaidia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks