Undani wa kilimo cha ‘Screen house’ Tanzania            

August 28, 2024 5:21 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni teknolojia rafiki inayowezesha kilimo cha mazao mengi ndani ya eneo dogo.
  • Uwekezaji wa teknolojia unahitaji mtaji mkubwa usiopungua Sh12 milioni kwa eneo la ukubwa wa mita 12 kwa 20.
  • Ni fursa ya kuongeza ‘maokoto’ kwa wakulima.                   

Arusha. Licha ya muda kuyoyoma na mamia ya wahudhuriaji wa Nane Nane kuanza kutoka, baadhi wanaonekana kuingia katika viwanja vya maonesho hayo mkoani Arusha kujionea teknolojia adimu za kilimo, ufugaji na uvuvi. 

Miongoni mwa watu wanaoingia katika viwanja vya Nane Nane vilivyopo Themi- Njiro yalipokuwa yanafanyika maonesho hayo kwa kanda ya kaskazini ni Theresia Mosha anayeonekana kuvutiwa na teknolojia ya kilimo inayoizuia mimea dhini ya jua, upepo na wadudu. 

Teknolojia hiyo, inayohusisha kulima ndani ya eneo moja lililofunikwa kwa neti na karatasi ngumu kuzuia jua, upepo na wadudu waharibifu, humuwezesha mkulima kulima mazao mengi yenye viwango na ubora unaotakiwa katika soko la kimataifa.

Teknolojia hiyo, iliyomfanya Theresia ashindwe kujizuia na kusogelea banda la banda la kampuni ya Holand Greentech, inaitwa ‘Screen house’.

‘Screen house’ ni nini?

Unaweza kusema ni teknolojia kongwe iliyokosa umaarufu nchini Tanzania kutokana na uwepo wake kwa zaidi ya miaka 60 huku matumizi yake yakionekana kuwa mapya kwa wengi.

Screen house hujengwa kwa chuma kigumu (gravenile) kinachoweza kudumu kwa muda mrefu zaidi kikishikilia kingo za kitalu kilichozungushiwa karatasi ngumu kwa juu na neti laini inayowawezesha watazamaji kuona mazao kutokea nje.

Kwa ndani imetengenezewa matuta yaliyofunikwa kwa karatasi ngumu ya kutenganisha mazao na udongo pamoja na miundombinu ya umwagiliaji kwa njia ya mpira (drip irrigation) inayohakikisha uwepo wa unyevuunyevu na maji ya kutosha.

Licha ya kuonekana ni aina nyepesi ya kilimo isiyohitaji nguvu kazi kubwa kumwagilia, kupalilia pamoja na uangalizi, ujenzi wa teknolijia hii unahitaji utaalamu wa hali ya juu ambao unafanywa na kampuni rasmi zilizosajiliwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Afisa Kilimo wa Holand Greentech, Fahme Maulid anasema ni ngumu sana kupata matokeo tarajiwa iwapo mkulima ataamua kuitengeneza mwenyewe.

“Kuitengeneza hii kibongo bongo (bila kuhusisha watalamu) inawezekana ila naona tu utakuwa unakaribisha hasara kwa sababu hizi ‘material’ (malighafi) ni lazima utauziwa feki na zikaharibika ndani ya muda mfupi,” amesema Fahme.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo miongoni mwa mazao maarufu yanayolimwa katika kitalu hicho ni mbogamboga na matunda kama pilipili hoho za rangi, pilipili za kizungu (sweet pepper), tikiti tamu (sweet melon)  nyanya changa (cherry tomatoes) na matango.

Ili kupunguza uwezekano wa mazo kuharibika wakulima wanashauriwa kuweka karatasi ngumu itakayotenganisha udongo na mazao.Picha|Lucy Samson/Nukta Africa.

Ni fursa ya ‘maokoto’ kwa wakulima

Kwa wakulima wanaotamani kulima kisasa huku wakijiongezea kipato mwaka kwa mwaka teknolojia ya ‘Screen house’ ni miongoni mwa wanayoweza kuitumia.

“Niwahahakikishie wakulima ukitumia teknolojia ya ‘screen house ndani ya mwaka mmoja tu unaweza kupata ‘maokoto’ (mapato) ambayo kwa kilimo cha kawaida cha mbogamboga ingechukua muda mrefu kuyapata,” anasema Fahme.

Faida kubwa kwa mjibu wa Mtaalamu mwingine wa kilimo Ally Mfaume kutoka katika kampuni hiyo ni kwamba kilimo cha ‘screen house’ huwawezesha wakulima kulima mazao mengi bila kujali msimu hivyo kujihakikishia kipato mwaka mzima.

Mathalan pilipili hoho ambayo bei yake inazidi kupaa sokoni, Mfaume anasema kwa sasa imefikia kati ya Sh4,000 hadi Sh 6,000 huku mkulima akiwa na uwezo wa kuzalisha hadi mara tatu kwa mwaka katika eneo moja.

Fahme amefafanua kuwa ikiwa mkulima ataamua kulima zao la pilipili hoho pekee katika kitalu chenye uwezo wa kutoa matuta 10 na kwenye kila tuta akapanda wastani wa miche 20 anaweza kupata kilo 1,600 za zao hilo litakalomuingia Sh6.4 milioni ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

Faida hizo zinaweza kuongezeka zaidi ikiwa mkulima atalima eneo kubwa zaidi huku akilihudumia kwa kupiga dawa na kuchagua mbegu bora ikiwemo zinazouzwa na maduka mbalimbali ya pembejeo. 

“Hii ni teknolojia nzuri sana, miaka yangu yote ya ukulima sikuwahi kuisikia, nikipata tu mtaji wa kutosha nafikiri naweza kuwekeza kwenye aina hii yakilimo nimevutiwa sana,”  Theresia aliiambia Nukta Habari wakati akitazama screen house ya mfano.

Hata wakati wataalamu wa kilimo wakieleza faida za screen house baadhi ya wakulima wanasema si rahisi kwa mkulima wa kipato cha chini kujiingiza kwenye aina hiyo ya kilimo kutokana na kuhitaji uwekekezaji mkubwa mkubwa na mazao finyu.

‘Screen house’ huwezesha wakulima kuzalisha pilipili hoho kwa wingi huku zikiwa na ubora unaotakiwa katika soko la kimataifa.Picha|Lucy Samson/Nukta Africa.

Tatizo gharama

“Hii si mara yangu ya kwanza kuiona teknoljia hii…kwa sasa siwezi kuitumia kwa sababu mimi nalima huko vjijini na natamani nilime eneo kubwa nipate mazao mengi zaidi…

…kwa teknolojia hii nikitaka kulima eneo kubwa ni lazima niwe na mtaji mkubwa sana na kwa hali yangu siwezi kumudu,”anasema Kidai Kaisi mkulima mkoani Singida ambaye pia alitembelea maonesho ya Nane Nane mkoani Arusha.

Wadau wa kilimo wanaouza teknolojia hiyo wanakiri kuwa wakulima wengi wanavutiwa na teknolojia hiyo lakini wanashindwa kumudu gharama, jambo linapunguza tija katika uzalishaji. 

Ili kuwekeza kwenye kilimo hicho, mkulima anahitaji kuwa na Sh12 milioni hadi Sh17 milioni kwa eneo lenye ukubwa kati ya mita 15 kwa 20 hadi mita 17 kwa 20. Bei hii inahusisha ununuzi wa malighafi zikiwemo chuma zisizooza, ufundi na miundombinu ya umwagiliaji. 

Mbali na gharama wakulima wa screen house hukumbwa na changamoto ya masoko ambapo wanunuzi huwalazimisha kununua kwa kiroba jambo linalodidimiza wakulima.

“Changamoto kubwa tunayokutana nayo hapa ni masoko kama unavyojua soko la ndani walanguzi wanataka kununua kwa gunia wakati mazao yetu haya yakiuzwa kwa gunia ni kama hasara,” amesema Mfaume.

Mbali na kukosa soko, wakulima wa Screen house’ pia hutakiwa kufanya uchavushaji wa maua kwa njia ya mkono kutokana na kutokuwepo kwa wadudu wachavushaji kama nyuki na vipepeo. Hii huhitaji nguvu kazi kubwa kuhakikisha maua yete yamechavushwa ipasavyo ili kuleta matunda. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks