Tanzania yamuunga mkono Raila Odinga kuwania uwenyekiti wa kamisheni AU

August 27, 2024 7:35 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Rais Samia amwelezea kuwa ana uelewa wa kina kuhusu masuala ya maendeleo barani Afrika.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ameonesha wazi kumuunga mkono aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya Raila Odinga kwenye azma yake ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) akisema kuwa anaamini kiongozi huyo ana uwezo wa kuleta mabadiliko chanya kwa bara la Afrika. 

Rais Samia aliyekuwa akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kampeni ya kumnadi Odinga iliyofanyika Ikulu ya Nairobi kwa mualiko wa Rais wa Kenya, Dk William Ruto, amemwelezea Odinga kama kiongozi shupavu anaejua vyema kile ambacho AU inahitaji kufanya ili kukidhi mapungufu ya maendeleo yatakayokuza uwezo wa nchi washirika. 

“Tunataka kuona Umoja wa Afrika ukiwa na nguvu zaidi, ukipigania maendeleo ya kijamii na kiuchumi barani Afrika na kuhakikisha sauti ya Afrika inasikika vyema katika majukwaa ya kimataifa. Ni kwa kufikia malengo haya tutakuwa tumewatendea haki mashujaa wetu waliojitolea kupigania uhuru wa kisiasa, utu wa mwanadamu, na ukombozi wa kiuchumi…

…Kutokana na hali hii Tanzania inaihakikishia Kenya kwamba inaunga mkono kikamilifu ugombea wa Odinga,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameongeza kuwa Odinga ana uelewa wa kina kuhusu masuala ya maendeleo barani Afrika ndio maana alipewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa miradi ya miundombinu, jukumu ambalo amelifanya kwa weledi mkubwa. 

“Tunajua kuwa kwa uongozi wake, Umoja wa Afrika utaweza kutimiza malengo yake ya kuendeleza miundombinu na kuimarisha uchumi wa bara letu.” Ameongeza Rais Samia

Umoja wa Afrika unamelengo ya kuimarisha umoja na mshikamano wa nchi za Afrika, kulinda uhuru na haki za kujitawala, kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kukuza amani na usalama, na kuhimiza haki za binadamu na utawala bora. 

Pia, Umoja wa Afrika unalenga kukuza ushirikiano wa kikanda na kimataifa, kutetea maslahi ya Afrika duniani, na kuhakikisha ushiriki wa bara katika masuala ya kimataifa. 

Rais Samia amebainisha kuwa ili Umoja wa Afrika utimize malengo uliyojiwekea unahitaji ushindani kwenye mageuzi ya kitaasisi na kuimarisha uwajibikaji, kuimarisha umoja kwa kusitisha vita na mapigano na kuendesha ajenda ya maendeleo ya Afrika.

Kwa mujibu wa Odinga, bara la Afrika linasumbuliwa na mapigano na vita, njaa, umaskini, kuongezeka kwa mabadiliko ya tabia ya nchi, ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, magonjwa ya kuvuka mipaka na maambukizi.

“Ninapanga kufanya kazi na nyinyi wakuu wa nchi kuifanya AU kutumikia maslahi ya Waafrika wengi wasio na sauti…iwapo nitachaguliwa kuwa mwenyekiti ninapendekeza kutumia kipindi cha mpito kuchambua kwa kina mapendekezo yaliyopo ya mageuzi na kujenga uwezo wa tume ya AU, lengo kuu ni kufuatilia utekelezaji wa ripoti zilizotungwa hadi sasa,” amesema Raila 

Rais Samia amehitimisha hotuba yake kwa kusema, “Kwa pamoja, Tanzania inasema Baba (Odinga) anatosha, achaguliwe.”

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Afrika, akiwemo Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni; Rais wa Sudan Kusini, Mhe. Salva Kiir Mayardit; na Waziri Mkuu wa Burundi, Mhe. Gervais Ndirakobuca, pamoja na viongozi wengine kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na kwingineko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks