Serikali kuwawezesha watafiti kuzalisha chanjo

August 31, 2024 5:26 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Zaidi ya Sh2 bilioni zimetengwa kuiwezesha taasisi Nimr kufanya utafiti wa dawa za asili.
  • Serikali yatamani watafiti hao kuzalisha angalau chanjo moja ya magonjwa katika mwaka huu wa fedha.

Mwanza. Serikali kupitia Wizara ya Afya nchini imepanga kuziwezesha taasisi za utafiti nchini kubuni dawa tiba ikiwemo chanjo za magonjwa mbalimbali yanayohatarisha afya za Watanzania.

Kauli hiyo ya Serikali inakuja wakati Tanzania na nchi nyingi barani Afrika zikikabiliwa na ugonjwa wa MonkeyPox unaosababisha vifo huku kukiwa na uhitaji mkubwa wa chanjo hususan katika nchi zilizoathirika na ugonjwa huo.

Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel aliyekuwa akizungumza kwenye kongamano la tatu la kisayansi la tiba asili lililofanyika Jijini Mwanza, leo Agosti 31, 2024 ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) pamoja na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuhakikisha inawasaidia waganga hao katika kufanya tafiti hizo.

“Kwa miaka mitatu sasa Serikali inatenga fedha kwa ajili ya kufanya utafiti kwenye dawa za asili ambapo dawa za aina mbalimbali zinachunguzwa na mpaka sasa zipo baadhi ya hospitali zimeruhusiwa kutumia dawa hizo…

…Lakini kama wizara tunatamani kuona kati ya tafiti za dawa asili zitakazofanyika kwenye mwaka huu wa fedha iwepo na dawa tiba ya chanjo ya asili ambayo inaweza kutumika katika kutibu ugonjwa wowote  na dawa hiyo itatambulishwa ulimwenguni,” amesema Dk Mollel.

Aidha, Dk Mollel amewataka waganga hao kuacha kutumia hisia na imani potofu linapokuja suala la matibabu badala yake wazingatie utaalamu, ufanisi na usalama uwezo wa dawa katika kutibu.

“Ili kuifanya tiba asili iwe kwenye mfumo wa kisayansi waganga wanatakiwa kuacha imani za ajabu kwa kuwa zinadhoofisha utaalamu wa tiba hizo,”amesema Dk Mollel.

Awali, Mkurugenzi mkuu wa Nimr, Profesa Said Aboud amesema zaidi ya Sh2 bilioni zimetengwa kuiwezesha taasisi hiyo kufanya utafiti wa dawa za asili zitakasaidia kutibu magonjwa mbalimbali.

Prof Aboud ameongeza kuwa fedha hizo zitatumika kufanya tafiti zitakazojumuisha huduma jumuishi ikiwa ni maelekezo ya utekelezaji wa huduma za afya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini, Profesa Hamis Malebo ameiomba Serikali iwekeze kwenye taasisi ya utafiti  kwa kupewa fedha za kuwa wanafanya utafiti wa kuhakiki uwezo na usalama wa dawa za asili ambazo zinatumika na Watanzania ili ambazo zinakidhi vigezo ziingizwe kwenye mfumo wa afya.

Malebo amewaambia wahudhuriaji wa kuwa Wizara ya Afya inatakiwa kutoa kipaumbele kwenye bajeti ya Nimr kwenye jukumu la kubaini uwezo na usalama wa dawa walizotumia mababu na mababu ili ziingizwe kwenye mfumo wa sayansi kwakuwa nyingi zimebainika kuwasaidia watanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks