Zifahamu faida, hasara za hadhi maalumu, uraia pacha

June 21, 2023 9:47 am · David
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali ya Tanzania yasema itaanza kutoa hadhi maalumu mwaka ujao wa fedha 2023/24
  • Uamuzi huo umepokelewa kwa maoni tofauti na Watanzania na diaspora
  • Wachambuzi watoa faida na hasara za hadhi maalumu na uraia pacha

Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imebainisha kuwa ipo mbioni kukamilisha mchakato wa kutoa hadhi maalumu kwa diaspora wenye asili ya Tanzania na uraia wa nchi nyingine katika mwaka ujao wa fedha wa 2023/24 ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo nchini.

Mchakato wa kutoa hadhi maalumu kwa diaspora umekuwa ukizungumzwa toka mwaka 2021, Serikali ilipoweka wazi msimamo wake kuwa itatumia mfumo huo badala ya uraia pacha jambo ambalo halikuungwa mkono na watu wote.

Dk.Stergomena Tax ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alipokuwa akisoma hotuba ya bajeti ya wizara hiyo Mei 30, 2023 aliwaambia wabunge kuwa hadhi maalumu hiyo imejumuisha mambo yote muhimu ambayo diaspora waliyaainisha.

Hata hivyo kutokana na kuwepo kwa  mapokeo tofauti ya wadau kuhusiana na hadhi maalumu, Nukta habari imefanya mahojiano na mchambuzi wa siasa za kitaifa na kimataifa Maggid Mjengwa ambaye amefafanua maana ya hadhi maalumu, faida na hasara zake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Stergomena Tax alipokuwa akisoma bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24 bungeni jijini Dodoma. Picha| Wizara ya Mambo ya Nje

Hadhi maalumu ni nini?

Kwa mujibu wa Mjengwa hadhi maalumu ni hati au utambulisho unaomuwezesha mtu mwenye uraia wa nchi nyingine kupata baadhi ya huduma kama wanazopata raia wa nchi husika ikiwemo, kuishi nchini humo bila viza, kumiliki mali pamoja na kuwekeza.

Kwa msingi huo ina maana diaspora wenye asili ya Tanzania ama nchi nyingine sasa wataweza kufanya uwekezaji kama biashara na kumiliki ardhi, kurithisha watoto wao mali, pamoja na kufanya kazi katika baadhi ya sekta.

Hata hivyo hadhi maalumu haimpi fursa mhusika kufaidi haki zote kama za raia kamili wa nchi hiyo, kwa mfano haki ya kushiriki shughuli za kisiasa yaani kugombea au kupiga kura.

Kwa mujibu wa Waziri wa Katiba na Sheria, Damas Ndumbaru mtu mwenye hadhi maalumu hawezi kushiriki shughuli za kisiasa kwa sababu mtu huyo ni raia wa nchi zaidi ya moja.

“Chukulia mfano mimi niwe na uraia wa nchi tatu na ni kiongozi, uaminifu wangu utakuwa kwa nchi gani, kwa sababu ukinipa fursa ya kisiasa naweza kuwa mpaka Rais, je Watanzania wanaikubali hiyo?,” anauliza Damas Ndumbaru.

Uraia pacha

Kwa mujibu wa Mjenga hii ni aina ya uraia ambapo mtu anaweza kupata haki zote za  kiraia kwa nchi zaidi ya moja kwa wakati mmoja.

Mathalani kama mtu ana uraia wa Marekani na Kenya basi anaweza kupata haki zote za raia wa Kenya akiwa nchini humo na anaweza kupata zote za raia wa Marekani akiwa huko.

Faida za mfumo huo wa uraia ni mtu kuwa na uwezo wa kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya mataifa yote mawili kwa nyakati tofauti, pamoja na kufaidi fursa zinazotolewa ikiwemo za kielimu, kiuchumi, kijamii pamoja na kisiasa.

Hata hivyo pamoja na faida hizo unaweza kukumbana na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kukatwa kodi mara mbili, pamoja na kukosa ajira katika baadhi ya nafasi ambazo kuwa raia wa nchi mbili ni kigezo cha kutopata kazi hiyo.

Sheria ya Tanzania inasemaje

Kwa mujibu wa idara ya uhamiaji, uraia wa Tanzania inaongozwa na Sheria ya Uraia ya Mwaka 2002 pamoja na kanuni zake za mwaka 1995 ambao ni uraia wa kuzaliwa, uraia wa kurithi pamoja na uraia wa tajinisi.

Raia wa kuzaliwa ni yule ambaye amezaliwa nchini Tanzania ambapo mmoja wa wazazi wake akiwa mtanzania, huku uraia wa kurithi ni ule ambao mtu huzaliwa nje ya Tanzania na mzazi mmoja au wote wakiwa ni raia wa Tanzania.

Uhamiaji wamebainisha kuwa raia wa tajinisi ni raia wa nchi nyingine kwa asili lakini aliomba kuwa raia wa Tanzania baada ya kuishi nchini kwa muda wa kuanzia miaka 10 pamoja na kukidhi baadhi ya vigezo vinavyohitajika.

Kwa maamuzi ya Serikali ya kutoa hadhi maalumu kwa Diaspora sasa Tanzania inaungana na mataifa kama India pamoja na Ujerumani ambayo huwapa raia wa nchi nyingine wenye asili ya nchi hizo utambulisho maalumu.

Zaidi ya mataifa 16 barani Afrika yanaruhusu uraia pacha ikiwemo ambapo kwa Afrika Mashariki Kenya na Burundi zimekuwa zikitolewa mfano na baadhi ya Watanzania na Diaspora wanaotamani uraia pacha.

Enable Notifications OK No thanks