Watahiniwa 111,056 wa kidato cha sita 2024 wafaulu mtihani, 22 wafutiwa matokeo

July 15, 2024 5:21 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ufaulu wa jumla waongezeka kwa asilimia 0.20.
  • Ufaulu wa wanawake na wanaume wapishana kiduchu.

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha sita 2024 ambapo watahiniwa 111,056 wa shule na kujitegemea wenye matokeo ya mtihani huo wamefaulu huku 22 wakifutiwa matokeo.

Idadi hiyo ni sawa na asilimia 99.43 ya watahiniwa wenye matokeo waliofanya mtihani huo. 

Katibu Mtendaji wa Necta Dk Said Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo hayo leo Julai 13,2024 Visiwani Zanzibar, amesema ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 0.20 ikilinganishwa na mwaka 

“Wanawake waliofaulu ni 49,837 sawa na asilimia 99.6 wakati Wanaume waliofaulu ni 61,219 sawa na asilimia 99.28, mwaka 2023 watahiniwa waliofaulu walikuwa ni 104,549 sawa na asilimia 99.23, hivyo ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 0.20 ikilinganishwa na mwaka 2023” amesema Dk Mohamed.

Necta imebainisha kuwa watahiniwa wa shule waliofaulu ni 103,252 sawa ambapo wanawake ni 46,615 sawa na asilimia 99.93 na wanaume ni 56,637 sawa na asilimia 99.91 huku wale wa kujitegemea wakiwa  7,804.


Soma zaidi:Matokeo ya kidato cha sita 2024 haya hapa


22 wafutiwa matokeo

Wakati wanafunzi wakifurahia matokeo yao Necta imewafutia matokeo watahiniwa 22 ambapo 17 ni wa shule na 5 wa Kujitegemea kutokana  na kufanya udanganyifu katika mitihani.

Dk Mohamed amebainisha kuwa udanganyifu huo ulifanywa na wananfuzni wenyewe wakiwa ndani ya chumba cha mtihani na hauhusishi shule wala vituo vya mtihani.

“Udanganyifu huu ni wa watahiniwa wenyewe,wapo ambao waliingia na simu, wapo walikutwa na “notes”, wapo ambao walisaidiana nakupasiana ‘booklet’ (kitabu cha kujibia mtihani) ndani ya chumba cha mtihani, hizi ni aina mbalimbali za udanganyifu ambazo zote zinapelekea matokeo kufutwa,”amesema Dk Said.

Dk Mohamed ameeleza kuwa matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 (2) (i) na (j) cha sheria ya Baraza la Mitihani sura ya 107 kikisomwa pamoja na kifungu cha 30(2) (b) cha Kanuni za Mtihani Mwaka 2016.

Hata hivyo, Dk Mohamed hajaweka wazi ikiwa zipo shule zilizofungiwa kutokana na udanganyifu kama inavyojitokeza katika matokeo ya miaka mingine.

Enable Notifications OK No thanks