Serikali kuongeza mabasi 100 ya mwendokasi

July 15, 2024 2:33 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Mabasi hayo yatanunuliwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya NMB

 Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema inatarajia kuongeza mabasi 100 ya mwendokasi ili kutatua changamoto ya usafiri jijini Dar es Salaam.

Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu allyekuwa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo Julai 15, 2024 amesema kuwa mabasi hayo yatanunuliwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya NMB.

“Kwa kipindi cha miezi miwili nimekuwa nikifanya vikao na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart), Kampuni ya Mabasi Yendayo Haraka (Udart), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) na nafikiri kwa sasa tumefikia ukingoni maana tumeona inaenda kuleta crisis (maafa) na kuathiri taswira nzuri ya Serikali,” amesema Mchechu.

Kwa mujibu wa Mchechu mabasi hayo yatakuwa yamewalisi nchini ndani ya miezi sita ijayo ili kusaidia kutatua changamoto ya usafiri wa mabasi yaendayo kasi.


Soma zaidi: Zifahamu nauli mpya mabasi yaendayo haraka, teksi mtandao


Kauli ya Mchechu imekuja wakati kukiwa na malalamiko kwa wadau na wananchi juu ya ubora wa mabasi hayo kutokana na mlundikano wa watumiaji pamoja na uchache wa usafiri huo kulinganisha na mahitaji yaliyopo.

Mbali na changamoto hizo baadhi ya mabasi hayo pia yana miundombinu chakavu hatua inayotajwa kutokidhi mahitaji wa watumiaji ikiwemo wenye ulemavu na wazee.

Ili kutatua changamoto hizo Mchechu amesema ni muhimu sana kwa mji kama Dar es Salaam kuwa na kampuni za usafiri zaidi ya moja zitakazosaidiana kutoa huduma hiyo kwa wananchi.

Kugombania usafiri, kubanana ni sehemu ya maisha ya wakazi wa Dar es Salaam waliochagua kutumia mabasi ya mwendokasi kama nyenzo ya usafiri.Picha|Uhuru Media.

Itakumbukwa kuwa Oktoba 24, 2023 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed  Mchengerwa aliuelekeza uongozi wa Dart kuongeza watoa huduma ili kuboresha huduma ya usafiri huo.

Aidha, Mchechu ameitaka Dart ifikapo Agosti mwaka huu kuhakikisha wametengeneza mifumo ya ukusanyaji fedha ili kudhibiti mapato na kupunguza wizi. 

“Kuna wizi mwingi unafanyika kwenye cash, mimi huwa nasema ni ‘headache’ kusimamia huu mradi kwenye suala la malipo. Tumekubaliana na Dart kuwa hadi Agosti 2024 wawe wamekamilisha mfumo wa nauli kwa njia ya mtandao.” amesema Mchechu.

Enable Notifications OK No thanks