Fisi: Mnyama wa ajabu kuliko tunavyodhani

September 20, 2021 9:25 am · Nasibu
Share
Tweet
Copy Link
  • Jambo moja la kushangaza ni kwamba fisi anaweza kula fisi mwenzie.
  • Akiona windo jipya hujitapisha ili kula chakula kingine.
  • Fisi jike na fisi dume wote wawili wana uume.

Inajulikana kwamba fisi akishika windo lake haachi kitu, anakula kuanzia kichwa hadi kwato. 

Dah! Hongera zake kwa kweli, maana mimi kila nikiwaza ng’ombe anapochinjwa kuna viungo vyake vingi huwa havifiki mezani, fisi amethibiti upotevu usiyo na tija, wazungu wanaita ‘total diet.’

Hata asiyemjua fisi atakuambia jinsi mnyama huyo alivyopewa sifa ya kula kwenye hadithi na vitabu vingi lakini kama umekuja hapa kusoma hii makala, basi amini kwamba kuna mengi zaidi yatakayokuacha mdomo wazi.

Binafsi kuandika tu hii makala, nikajikuta namshangaa fisi kama simjui vile wakati nishabumiana naye mbugani mara nyingi tu, ni muoga tu hana lolote.

Fisi ni mnyama jamii ya paka, ana ngozi ya njano kahawia mpauko yenye mabaka meusi. Hupenda kula wanyama wengine na huwinda kwa makundi.

Fisi kala fisi!

Jambo moja la kushangaza ni kwamba fisi anaweza kula fisi mwenzie. Kama vitoto vimezaliwa afu ndiyo njaa imetawala basi hao ni chakula cha baba, kwani shida iko wapi? Si watazaa tu wengine.

Akilipania windo hakubali kushindwa kirahisi, lazima atalipata. Picha| The Global Alliance of National Parks.

Fisi katapika

Fisi kala kashiba kalala. Mara ghafla wanakikundi wenzake wamekamata nyumbu. Huyo fisi ataamka, atajitapisha chakula alichokula ili apate nafasi ya kula nyumbu. Ndo maisha ya fisi hayo, mdomo ukiwa bize basi kwake yeye ndo kasha-win maisha.

Jike ndiyo masta

Fisi jike ndiye mbabe kuliko dume na ana umbo kubwa na ni mkali zaidi ikija kwenye uwindaji. Fisi jike na fisi dume wote wawili wana uume. 

Fisi wanapojamiana, uume wa dume huingia ndani ya uume wa jike. Uume huo wa jike hutumika pia kwenye uzazi na huishia kuchanika wakati anazaa.

Mtoto wa fisi anaweza kupoteza maisha kwa kukosa hewa wakati anapitishwa kwenye uume huo.

Fisi jike ana chuchu mbili tu ambazo watoto hugombania kunyonya hadi kuuana. Yaani mtoto wa fisi anapitia shuruba nyingi sana mpaka anakuja kuwa mkubwa na ndiyo maana hawezi kukubali kufa kizembe eti fisi afe kwa njaa, kweli! 

Yuko radhi hata ale viatu vya ngozi vilivyosahaulika na watalii, fisi anajitosa tu.

Fisi ni wanyama wa usiku, wanaishi kwenye nyasi, misitu, vichaka, jangwani na hadi milimani.

Wanyama hao ni waoga lakini umoja wao huwafanya kumshinda adui kwa urahisi na kula nyama yake bila kusaza kitu. Picha| Wallpaper Frale.

Fisi hutumia sana akili

Wanasema fisi ana uwezo wa kufikiria kuliko sokwe. Hupenda kuiba mayai ya wanyama wengine kama mbuni. Yai la mbuni huwa ni ngumu kwa yeye kulipasua kwa meno yake hivyo basi hutafuta bonde lenye mawe au miamba na yeye akiwa kwenye mwinuko ataliachia yai hilo literemke na kupigiza kwenye mawe na miamba.

Hufanya hivyo mara nyingi mpaka yai lipasuke ili aweze kula kilichopo ndani. Fisi hashindwi kwenye kula.


Fisi anacheka!

Ukisikia kicheko porini amini kwamba hapo kuna hatari. Fisi hucheka kama mshangao akiona chakula. Fisi huwinda kwa makundi na fisi mwenye kicheko kikali zaidi ndiyo kiongozi wa kundi na mara nyingi kundi huongozwa na fisi jike.

Fisi dume hutimuliwa kwenye familia akishafikia balehe na hapo ndipo hujiunga na kundi la uwindaji na ni lazima apigane na fisi dume wa kundi hilo na muda mwingine hupigana hadi kupoteza maisha.


Fisi ni muoga sana

Akiwa peke yake, fisi hana ujanja mwingi. Fisi hula watoto wa wanyama karibu wote uwajuao, kuanzia simba, chui, tembo hadi kifaru kwa sababu ana uwezo wa kuwamudu ila wakiwa kikundi wanakuwa na nguvu sana na kujiamini. Kundi la fisi linaweza kupigana na kundi la simba bila uwoga kabisa.

Tukutane mnara

Fisi hufanya mikutano ya kuwasiliana ambayo majike na madume wote huudhuria huku uume zao zikiwa zimesimama. Wanasayansi wanaamini kwamba uume wao huwasaidia kuwasiliana. Binafsi, naomba huu uwe mjadala mpana wa siku nyingine tafadhali. Ahsante

Zamani fisi walikuwa wanahushishwa na ushirikina kwamba wachawi kuwapanda kama farasi na kuwatumia kama usafiri wakienda kuiba watoto wa mifugo. 

Fisi wanapatikana karibu kila mbuga hapa nchini na kama tulivyosema hapo awali, fisi huishi kwenye nyasi, misitu, vichaka, jangwani na hadi milimani. Tembelea Ngorongoro ujionee kwa macho yako mishemishe za fisi kutafuta mawindo mbugani.

Nasibu Mahinya ni mjasiriamali na Afisa Masoko wa soko la mtandaoni la utalii la TenTen Explore nchini Tanzania. Amekuwa mdau muhimu wa shughuli za utalii zinazofanyika ndani na nje ya Hifadhi za Taifa. Unaweza kumpata kupitia tovuti yake ya www.nasibumahinya.com.

Enable Notifications OK No thanks