Nchimbi ahimiza utulivu Serikali ikiwasaka watekaji

September 13, 2024 4:11 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Akiri kuwepo matukio ya utekaji, upoteaji, mauaji na kuwataka wananchi kutoa muda wa kutosha uchunguzi kufanyika.
  • Viongozi wanaoibua taharuki kushughulikiwa.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Emmanuel Nchimbi amewaasa wananchi na wafuasi wa vyama vya siasa nchini kuwa na utulivu ili kutoa muda wa kutosha kwa vyombo vya usalama kufanya uchunguzi kuhusu matukio ya utekaji na mauaji yaliyoripotiwa nchini.

Kauli ya Nchimbi inakuja siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia kwa Mwenyekiti wake Freeman Mbowe kubainisha kuwa wanakusudia kuandamana Septemba 23, 2024 kuishinikiza Serikali kuwajibika kwa vitendo hivyo ambapo tayari Jeshi la Polisi limeshayapiga marufuku maandamano hayo.

Hivi karibuni kumeripotiwa matukio kadhaa ya utekaji na mauaji baadhi yakihusisha wafuasi na viongozi wa vyama vya upinzani akiwemo Ally Kibao ambapo kwa mujibu wa Chadema aliuawa baada ya kutekwa kwenye basi la Tashriff akiwa safarini kuelekea Tanga kutokea Dar es Salaam Septemba 6, 2024 na mwili wake kuokotwa kesho yake ukiwa na majeraha.

Aidha, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika taarifa yake ya Agosti 9, 2024 iliyokemea vitendo vya utekaji na upoteaji imebainisha  kuwa vitendo hivyo vimeathiri jumla ya watu 82 tangu mwaka 2016 ambao baadhi walipatikana na majeraha au kutopatikana kabisa huku wengine wakikutwa wamefariki.

Nchimbi aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Septemba 13, 2024 amesema CCM inatambua hali hiyo na imekasirishwa na matukio ya utekaji lakini uchunguzi wa matukio hayo unapaswa kupewa muda wa kutosha ili kupata matokeo sahihi yenye haki kwa pande zote.

“Chama chetu kimekasirishwa na kwa kweli tunataka Serikali iharakishe uchunguzi huu na matukio ya namna hii kwa kweli yakomeshwe. Lakini pia tunasisitiza kwa wananchi wa Tanzania kutoa muda wa kufanya uchunguzi, tuhakikishe kwamba maamuzi tunayoyafanya yanatenda haki,” amesema Nchimbi jijini Dar es Salaam.

Nchimbi ameongeza kuwa haki ya kusikilizwa inapaswa kuzingatiwa na kwamba uchunguzi unapaswa kufanywa kwa kina ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu asiye na hatia anayeadhibiwa kwa makosa ambayo hakuyatenda.

“Kuna haki ya kusikilizwa na uchunguzi wa kina ili usije ukamuonea mtu asiyehusika, lazima kama Taifa tufanye kila njia kuhakikisha raia wetu wote wanatendewa haki, lakini vilevile tuhakikishe mtu yeyote anayetuhumiwa kwa kosa asionekane mkosaji mpaka uthibitisho umetolewa,” amesema Nchimbi.

Viongozi wanaoibua taharuki kushughulikiwa

Nchimbi amekiri kuwa kauli za baadhi ya viongozi wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) zimechangia kuibua hisia kuwa chama hicho kinahusika na matukio hayo ya utekaji.

Ameongeza kuwa kwa sasa wameanzisha jitihada za kushughulikia viongozi wanaotoa  kauli hizo kupitia kamati za maadili. 

“Kauli kauli za viongozi wetu hasa wa UVCCM wakati mwingine zinafanya watu waamini kwamba wanahusika kwenye mambo haya (utekaji) la kwanza sisi tunachukua hatua, wengine wanaitwa kwenye kamati za maadili, wengine wanapewa adhabu kwa kauli za kijingajinga,” amesema Nchimbi.

Aidha, kiongozi huyo amebainisha kuwa huenda Serikali ikahitaji msaada wa wataalamu wa nje kufanya uchunguzi wa vitendo hivyo vya utekaji na wao kama chama watauunga mkono uamuzi huo ili kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria. 

“Hatuna tatizo na njia itakayotumika kuwapata, tunataka wapatikane wachukuliwe hatua za kisheria mambo haya yakomeshwe,” amesisitiza Nchimbi alipokuwa akijibu maswali aliyoulizwa na wanahabari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks