Mila, desturi zinavyokwamisha wanawake kugombea nafasi za uongozi Longido

September 11, 2024 6:05 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na mfumo dume unaozuia wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
  • Serikali, LSF waungana kutoa mwangaza.

Arusha. Ikiwa imesalia miezi michache kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba mwaka huu, baadhi ya mila na desturi zimeendelea kukwamisha wanawake wa jamii za Kimasai kugombea katika nafasi hizo.

Kwa miaka mingi wanawake wa jamii za kifugaji ikiwemo Wamasai waishio mkoani Arusha wameendelea kukumbana na mila na desturi zinazowazuia kufanya maamuzi hasa ya kugombea katika nafasi mbalimbali za uongozi hali inayopunguza ujumuishi kijinsia katika ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa.

Upendo Ndorosi Diwani wa Viti Maalum (CCM) kutoka Tarafa ya Longido aliyekuwa akizungumza katika mkutano uliokutanisha wanawake wa jamii za Kimasai katika tarafa hiyo na wadau wa Asasi za Kiraia leo Septemba 11,2024 amesema miongoni mwa mila na desturi hizo ni pamoja na mfumo dume ambao unawazuia wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

“Wanawake katika tarafa yangu ya Longido wana changamoto kubwa ya mfumo dume, akichukua fomu ya kugombea uenyekiti wa Serikali za Mtaa ataulizwa anajua ng’ombe wanapopelekwa kupata malisho?….

…Wanaume wengine wanasema wanawake wakienda kuichukua fomu tutawapokonya na tutawapiga, amesema Diwani Upendo.

Kutokana na hali hiyo Upendo anasema ushiriki wa wanawake kugombea nafasi za uongozi ni mdogo ambapo wengi wao wanasubiri tu kuteuliwa.

“Hali ya kisiasa kwa sisi wanawake wa jamii ya kimasai bado ni ngumu tupo sisi ambao tupo lakini tunapewa nafasi za viti maalum, kugombea nafasi za diwani wa kata, uenyekiti wa kijiji bado ni changamoto,” amesema Upendo.

Wanawake wa jamii ya Kimasai wakiwa kwenye picha pamoja na wadau wa Asasi za Kiraia waliotembelea mradi wa wanawake tunaweza uliopo Kata ya Longido jijini Arusha. Picha/ Lucy Samson/ Nukta Africa.

Serikali, LSF waungana kutoa mwangaza

Kutokana na uwepo wa changamoto hizo Upendo kwa kushirikiana na viongozi wengine wa Serikali pamoja na azaki ya Legal Service Facility (LSF) wameanza kutoa elimu na mafunzo wezeshi kwa wanawake wilayani Longido hali ilinayoongeza uelewa na ari ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Kwa sasa Serikali na LFS wanawaandaa wanawake 12 kugombea katika nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa huku wanawake wengine wakiwezeshwa kuzitambua haki zao, kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazowaingizia kipato na wengine wakiruhusiwa kumiliki ardhi.

Wanaume nao hawajasahaulika katika mapambano dhidi ya mila hizo ambapo na wao wamepewa elimu iliyowezesha kuundwa kwa kikundi cha mashujaa wanaopigania haki za wanawake na kuhamasisha wanaume kuachana na mila kandamizi.

“Tunaendelea kuhamasisha wazee wenzetu ili waweze kuwaruhusu wanawake kutoka majumbani na kufanya shughuli zao…tukiwapa wanawake nafasi ya uongozi wanafaa sana,” amesema Lukas Simbeke kiongozi wa mila wa Kimasai (Leigwanan).

Kwa mujibu wa Simbeke uhamasishaji huo hufanyika katika vikao vya viongozi wa mila katika ngazi za familia, ukoo hata vijiji na wamejipanga kufikia maeneo mengi zaidi ili kutokomeza mila na desturi hizo zinazowakandamiza wanawake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks