Mganga wa kienyeji sasa atuhumiwa mauaji ya watu 10 Tanzania

August 28, 2024 6:43 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Miili 9 yakutwa imezikwa ikiwa imekalishwa kwenye shimo kwenye makazi ya mganga huo huku mmoja ukiokotwa pori la akiba. 

Dar es Salaam. Uchunguzi wa Jeshi la Polisi unaoendelea katika baadhi ya kesi za watu kupotea nchini umebaini kuwa mganga wa kienyeji anahusika kwenye tuhuma za mauaji ya watu 10 ambao sehemu kubwa ya miili yao ilizikwa kwenye makazi ya mtuhumiwa huyo katika mikoa miwili tofauti. 

Siku tatu zilizopita Jeshi la Polisi lilieleza kuwa limemkamata mganga wa kienyeji aitwaye Nkamba Kasubi na wateja wake wawili Selemani Nyalandu na Said Msanghaa kwa tuhuma za mauaji ya watu watatu kwa sababu za kishirikina. 

Katika taarifa yake kwa umma, Msemaji wa Polisi, David Misime alisema miili ya watu hao watatu ilifukuliwa kwenye eneo la nyumba ya mganga huyo iliyopo kijiji cha Makuro wilaya Singida Vijijini mkoani Singida.

Miezi ya hivi karibuni kumekuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, wanaharakati, wanasiasa na wadau wengine wa haki za binadamu kuitaka polisi kuchunguza kwa makini matukio ya watu kutekwa na kupotea katika mazingira tatanishi. Baadhi ya wakosoaji wamekuwa wakilituhuhumu jeshi hilo kuhusika na matukio hayo, madai ambao polisi wameendelea kuyakanusha. 

Misime katika taarifa kwa umma leo Agosti 28, 2024 ameeleza kuwa polisi wamefukua 

miili zaidi ya marehemu sita kwenye nyumba nyingine ya mganga huyo iliyopo kijiji cha Porobanguma jijini Dodoma, huku mwingine ukiokotwa kwenye pori la akiba na kufikisha jumla ya miili 10 inayohusishwa na kesi za mtaalamu huyo wa jadi.

Miili hiyo mipya, kwa mujibu wa Misime imepatikana baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa wa nne aitwae Miraji Shabani aliyekuwa akijaribu kutoroka Agosti 25, kwa kutumia pikipiki ya mmoja kati ya watu ambao miili yao imepatikana baada ya kufukuliwa.

Mganga aonyesha miili saba zaidi

Baada ya kukamatwa kwake na kukutanishwa na watuhumiwa wenzake watatu ambao ni  Selemani Nyalandu na Said Msanghaa ndipo Kasubi akakubali kuwaongoza askari Polisi hadi kwenye mji wake mwingine tofauti na ule ilipofukuliwa miili mitatu ya awali na kuonyesha mashimo sita ambayo walifukia watu wengine waliowaua na kuwazika.

Miili iliyofukuliwa ilithibitisha kuwepo kwa marehemu Seni Jishabi (28) aliyeripotiwa kupotea tangu Machi 3, mkazi wa Porobanguma na kubainika kuwa aliuawa na kuzikwa Aprili 2024 na Mohamed Juma (27), mkazi wa Nyamikumbi A, Singida, aliyenyongwa na kuzikwa Mei 2024.

Misime amesema marehemu Daudi Msanku (27), ambaye pikipiki yake alikamatwa nayo mmoja ya watuhumiwa akijaribu kutoroka, alikuwa akiishi Gawidu mkoani Manyara. Msanku aliripotiwa kupotea Mei 27 na inadaiwa aliuliwa Mei mwaka huu na kisha mwili wake kuchomwa moto na majivu yake kuhifadhiwa kwenye ndoo. 

Marehemu mwingine ni Ramadhani Yusuph (26), mkazi wa Kidika, Manyara, aliyeuawa Aprili 2024.

Misime amesema miili mingine miwili imepatikana kwenye zizi la mifugo ikiwa ni ya watoto wa watuhumiwa waliokamatwa ambayo ni ya Mwekwa Kasubi, mtoto wa mganga aliyezikwa hai Machi 2023 akiwa na miezi 4 na Maka Nyalandu aliyeuawa na kuzikwa hai Juni 2023 akiwa na miezi 2.  

Mwili mwingine wakutwa pori la akiba

Vilevile, bosi huyo wa polisi amesema watuhumiwa hao walikiri kumuua Ramadhani Kilesa mzee wa miaka 80 aliyekuwa mkazi wa Porobanguma na kutupa mwili wake katika Pori la Akiba Swangaswanga ili mwili wake uliwe na wanyama pori licha ya lengo hilo kutotimia.

Kwa ujumla miili mitatu (3) imepatikana Singida na mingine saba (7) imepatikana mkoani Dodoma. Tofauti na mzee aliyetupwa porini, miili tisa (9) imekutwa imezikwa kwa kukalishwa kwenye shimo tofauti na ilivyo kwa mazishi ya kawaida, kwa mujibu wa Misime anayewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za kweli na sahihi kuhusu matukio hayo.

“Kila mmoja wetu tuelimishane kwa dhati, kwa kila mmoja kwa nafasi yake katika jamii ubaya na madhara ya kuendekeza imani za kishirikina, tamaa za mali bila ya kufuata maelekezo ya Mwenyezi Mungu, sheria za nchi na miiko katika jamii, kudhulumiana, kulipiza kisasi na wivu wa mapenzi,” amesema Misime. 

Kupatikana kwa miili hiyo huenda kukaanza kutoa ahueni kwa baadhi ya ndugu na jamaa ambao walipotelewa na wanafamilia bila kufahamu mahali walipo huku polisi wakishindwa kutoa majibu kwa wakati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks