Mchengerwa: Wanaoficha watoto wenye ulemavu wachukuliwe hatua za kisheria

September 17, 2024 7:43 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ataka kamati na ulinzi za usalama kufanya ufuatiliaji majumbani.
  • Aagiza kuimarishwa ulinzi kwa watoto wenye ulemavu kukabiliana na unyanyasaji.

Arusha. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mohamed  Mchengerwa amewataka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya nchini kuwachukulia hatua wazazi na walezi wote wanaoficha watoto wenye ulemavu majumbani na kuwazuia kupata elimu.

Mchengerwa aliyekuwa akizindua maadhimisho ya miaka 30 ya elimu jumuishi Tengeru, jijini Arusha leo Septemba 17,2024  amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa  kwa elimu hivyo wanaoficha watoto hawanabudi kuchukiliwa hatua za kisheria. 

“Ninawaelekeza wakuu wa mikoa wakuu wa wilaya kuanza kufatilia kubaini kama kuna mtoto mwenye changamoto amefichwa  ananyimwa haki ya elimu achukuliwe hatua mara moja,” amesema Waziri Mchengerwa.

Ili kufanikisha zoezi hilo Waziri Mchengerwa amezitaka kamati za ulinzi na usalama za mkoa kuanza ufatiliaji wa karibu majumbani kubaini watoto wenye ulemavu, kuwafanyia vipimo na kuwaandikisha katika shule za mahitaji maalum zilizopo karibu.

Kwa mujibu wa Mchengerwa Tanzania ina jumla ya shule 6,088 zenye mahitaji maalum kati ya hizo shule 309 zina mabweni kwa ajili ya wanafunzi wakike na wakiume huku kukiwa na shule mbili maalum kubwa za mfano kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum ikiwemo Shule ya Sekondari Patandi ambapo maadhimisho hayo yanafanyika 

Kuimarika kwa miundombinu hiyo kumechangia kuongeza uandikishaji wa watoto wenye ulemavu katika ngazi mbalimbali kutoka wanafunzi 28,422 mwaka 2022 hadi 78,429 mwaka 2024.

Ongezeni ulinzi wa watoto 

Katika hatua nyingine Mchengerwa ametaka viongozi hao wa mkoa na wilaya kuongeza ulinzi kwa watoto hususani wenye ulemavu dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyoendelea kuripotiwa nchini

“Ninaelekeza wekeni utaratibu kupitia kamati zenu za ulinzi na usalama ili kuhakiksha watoto wetu wanakuwa salama hatutaki kusikia pengine wamechukuliwa wamepeleka huku na huku na wengine wanafanyia vitendo ambavyo si vya kitanzania,” ameongeza Mchengerwa.

Mbali na usalama kwa makundi hayo Mchengerwa amesisitiza ulinzi kwa watanzania wote hususan katika kipindi hiki ambacho kuna taarifa za watu kutekwa na wengine kuuwawa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks