Dk Tulia: Serikali itazame upya kigezo cha umri ajira Tawa

September 2, 2024 5:27 pm · Bacley Madyane
Share
Tweet
Copy Link
  • Wabunge washauri umri uongezwe kutoka miaka 25 mpaka 30.
  • Lengo ni kutanua wigo wa vijana kupata ajira.

Dar es salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson ameishauri Serikali kupitia upya vigezo vya ajira vilivyowekwa na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (Tawa) kwenye ajira zake zilizotangazwa hivi karibuni ili kuongeza wigo wa vijana kuajirika.

Ushauri huo wa Spika Tulia umetokana na hoja ya dharura iliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ng’wasi Kamani aliyetaka wabunge waunge mkono hoja yake ya Serikali kuongeza umri kutoka miaka 25 hadi 30 kwa kuwa wahitimu wengi wako mtaani hawana ajira na zinazotoka ni chache.

Msingi wa hoja ya Kamani unatokana na tangazo la nafasi mbalimbali za ajira zilizotangazwa na Tawa ambapo miongoni mwa kigezo ni waombaji kutokuwa na umri wa zaidi ya miaka 25 kwa nafasi zote zilizotangazwa.

“Kigezo muhimu kwa waombaji wote hawa 351 ilikuwa ni kwamba wanatakiwa wawe kuwa na umri usiozidi miaka 25. Yaani awe na umri wa miaka 25 kushuka chini…

…Na vigezo vingine, kwa mfano kwenye udereva anatakiwa awe na vyeti vyote vya Veta na leseni, lakini awe na uzoefu wa mwaka mmoja wa udereva, kwenye hivi vingine wanatakiwa kuwa na vyeti vingine kama vile cheti, diploma au shahada,” amesema Kamani.

Hata hivyo, Kamani ameliambia Bunge kuwa vijana waliomaliza shule wasihukumiwe kwa kigezo cha umri, bali wahukumiwe kwa kigezo cha uwezo.

“Hawa watu tusiwahukumu kwa vigezo kama umri, tuwahukumu kwa uwezo kama wamemaliza na wako mtaani hawana kazi, kwa nini tuwahukumu kwa umri… 

…Kila mwaka wanaohitimu vyuo ni kuanzia wahitimu 100,000 hadi 300,000 na nafasi za kazi ni chache, mwanafunzi anapomaliza chuo umri hausimami, tuongeze walau ufike miaka 30,” amesema Kamani kwa msisitizo.

Wabunge waunga mkono

Baada ya kutoa hoja yake, wabunge mbalimbali wameichangia ambapo Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara amesema si sahihi kuweka ukomo wa umri kwa kigezo cha kushindwa kufanya aina ya mazoezi kwa kuwa wapo watu wenye umri mdogo na hawawezi kufanya mazoezi hayo. 

“Kuna watu wana umri wa miaka 25 hawawezi kuruka vihunzi, lakini wenye umri mkubwa wanaweza. Watu wengine ni watu wa mazoezi. Wao wangetoa bila kuweka kigezo cha umri, watu waombe kama ni suala la mazoezi mtu ashindwe huko.

“Ilivyokaa unaweka kizuizi mtu hawezi kuomba ile kazi na hana ajira nyingine na yuko mtaani, lakini umeweka umri kumbe angeweza kushinda. Suala la umri liondolewe ili isionekane ni ajira ya kundi fulani,” amesema Waitara.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda amesema kuweka umri wa miaka 25 kutawaweka vijana wengi nje, kwa kuwa ni muda mrefu ajira hazijatoka.

“Jeshi Usu linahitaji tu ukakamavu, tusogeze hadi umri wa miaka 30 na isiishie tu kwenye mambo ya Tanapa na tufanye na kwenye ajira nyingine, vinginevyo watoto wetu waliomaliza vyuo miaka sita iliyopita wataendelea kuachwa kwenye mfumo wakati wamesoma, suala la umri liongezwe kwenye ajira zote,” ameongeza Mwakagenda.

Spika Tulia apigilia msumari

Mara baada ya kusikiliza hoja za wabunge na kupitia tangazo la Tawa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliitaka Serikali kutoa ufafanuzi wa ulazima wa kigezo cha miaka 25 ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti na Utawala Bora George Simbachawene alikitolea ufafanuzi akisema umri ni muhimu kwa ajili ya kupima ukakamavu na uwezo wa kupokea mafunzo ya kijeshi.

“Tawa kwa uzoefu walionao na mahitaji ya nguvu kazi wanayotaka wanadhani umri wa miaka isiyozidi 25 unaweza kumuwezesha huyu mwanajeshi wanayemuandaa aende kupambana na mazingira kwenye utekelezaji wa majukumu yake,” amesema Simbachawene.

Hata hivyo, Spika Tulia ametupilia mbali hoja hiyo akisema utendaji kazi wa Tawa haufanani na majeshi mengine kama Jeshi la Polisi au Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) hivyo kigezo hicho hakina mashiko katika baadhi ya nafasi.

Aidha, Spika Tulia amelieleza Bunge jambo hilo si mara ya kwanza kujitokeza bungeni kuhusu vigezo vya ajira vinavyotolewa, kwenye maeneo ya jeshi na Jeshi Usu na kuwa yamewahi kujitokeza huko nyuma ambapo Bunge liliishauri Serikali kuondoa ulazima wa kigezo cha kushiriki mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika nafasi za ajira ili kutoa fursa kwa wale walioshindwa kupata mafunzo hayo kuomba ajira hizo.

“Nakumbuka tulisema kwa upande wa jeshi kwa sababu wana vigezo vya ziada waache hivvyo, na hizi taasisi nyingine ziangalie ambazo hazihitaji hiki kigezo cha watu kupitia mafunzo hayo,” amesema Spika Tulia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks