China, Tanzania, Zambia kuboresha reli ya TAZARA

September 4, 2024 5:14 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Zaingia makubaliano ya kuiboresha reli ili kuongeza ufanisi katika usafirishaji wa mizigo na abiria.

Dar es Salaam. Reli ya Tazara inatarajiwa kufanyiwa maboresho makubwa baada ya China, Tanzania na Zambia kusaini hati ya makubaliano ya kuiboresha reli hiyo ili kuongeza ufanisi wa uendeshaji mradi huo wenye zaidi ya miaka 50. 

Leo, Septemba 4,  Samia Suluhu Hassan, Rais wa China, Xi Jinping na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema walishuhudia uingiaji wa makubaliano hayo yaliyofanyika jijini Beijing, China, ikiwa ni moja ya hatua muhimu ya kuboresha reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,860. 

Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) ilijengwa na China miaka ya 1970 ikiwa ni mradi mkubwa zaidi kufanywa na taifa hilo barani Afrika ikianzia katika Bandari ya Dar es Salaam hadi Kapiri-Mposhi nchini Zambia.

Rais Samia ameeleza leo kwenye mtandao wa X zamani Twitter kuwa lengo kuu la awali la reli hiyo lilikuwa kuisaidia Zambia kupata huduma ya usafirishaji wa bahari kupitia Bandari ya Dar es Salaam wakati ambao nchi nyingine majirani zake zilikuwa chini ya utawala wa kikoloni.

Kwa kushirikiana na viongozi wa China na Zambia, Rais Samia amesema wamekubaliana kufanya maboresho ya reli ambayo kwa sasa inakabiliwa na uchakavu wa miundombinu. 

Uchakavu wa miundombinu na matatizo mengine ya kimtaji ni miongoni mwa masuala yaliyopunguza ufanisi wa Tazara kiasi cha kuathiri ratiba za safari za treni za abiria na mizigo. 

Mapema leo asubuhi abiria zaidi ya 200 walikwama kusafiri baada ya treni kushindwa kufanya safari kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya. 

Makubaliano hayo yaliyosainiwa Beijing ni sehemu ya ushirikiano mpana wa kiuchumi na kimaendeleo kati ya China na nchi za Afrika unaosisitizwa kupitia mkutano wa Forum on China-Africa Cooperation (FOCAC).

Rais wa Tanzania Samia Suluhu akimpa mkono wa pongezi Rais wa China, Xi Jinping baada ya kusaini makubaliano ya kuiboresha reli Tazara. Picha: Rais Samia Suluhu/X.

Rais Xi Jinping ameeleza kuwa China iko tayari kusaidia kufufua na kuboresha reli ya TAZARA ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji mizigo kutoka migodi ya Zambia hadi Bandari ya Dar es Salaam, hivyo kuchochea ukuaji wa kiuchumi na biashara katika ukanda huo.

Reli ya TAZARA, ambayo ni alama ya urafiki wa muda mrefu kati ya nchi hizi ina umuhimu mkubwa katika kuboresha uchumi wa kikanda na kuleta maendeleo kwa wananchi wake. 

Mapema Februari mwaka huu, China ilipendekeza kutumia Dola za Marekani bilioni 1 sawa na Sh2.6 trilioni kukarabati reli hiyo kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.

Hata hivyo, hadi sasa muda wa kuanza uboreshaji wa reli hiyo haujawekwa bayana na serikali hizo. 

Reli hii yenye njia moja, ilijengwa kati ya mwaka 1970 na 1975 kupitia mkopo usio na riba kutoka China, ikitoa njia ya usafirishaji mizigo kutoka kwenye migodi ya shaba na kobalti ya Zambia hadi pwani ya Tanzania na hivyo kuzuia utegemezi wa njia kupitia Afrika Kusini.

Shughuli za kibiashara za njia hiyo zilianza mwaka 1976, licha ya kupuuzwa na baadhi ya serikali za Magharibi wakati huo kama “reli ya mianzi”. 

Rais Xi Jinping, kupitia vyombo vya habari vya serikali, amenukukuliwa akisisitiza kwamba China iko tayari kuchukua fursa ya mkutano huu kufanya maendeleo mapya katika ufufuaji wa reli ya Tanzania-Zambia.

China yataka kuijenga Tanzania kuwa eneo la mfano

Aliongeza kuwa China inataka kushirikiana na nchi za Afrika Mashariki kuboresha mtandao wa usafiri wa reli na bahari na kuijenga Tanzania kuwa eneo la mfano kwa kuimarisha ushirikiano wa ubora wa juu wa Ukanda na Barabara.

Naye Rais Hakainde Hichilema wa Zambia aliipongeza China kwa msaada wake wa muda mrefu na kueleza matumaini yake kuwa makubaliano haya yataleta manufaa makubwa kwa Taifa lake.

Makubaliano ya kuboresha Reli ya TAZARA yanatarajiwa kuimarisha ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na abiria, kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa Kusini mwa Afrika. 

Kuboreshwa kwa reli hiyo ni kete nyingine ya ushindi kwa Rais Samia ambaye tangu aingie madarakani ameendelea kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu jambo ambalo limeendelea kuleta presha ya kifedha kutokana na miradi hiyo kutegemea zaidi mikopo. 

Baadhi ya wakosoaji vikiwemo vyama vya upinzani kwa nyakati tofauti wamesema ujenzi mfululizo wa miradi mikubwa unazidi kuongeza deni la Taifa ambalo lilifikia Sh91.7 trilioni hadi Machi 2024. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks