Bunge laazimia kutaifisha, kubatilisha umiliki wa shamba la Efatha Mlonje

August 27, 2024 10:30 pm · Bacley Madyane
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kamati maalum iliyoundwa na Dk Tulia Ackson kuwasilisha ripoti ya uchunguzi kuhusu mgogoro huo.
  • Wabunge wataka shamba hilo litaifishwe kulinda maslahi ya wananchi.

Dar es Salaam. Bunge la Tanzania limepitisha azimio la kutaifisha na kubatilisha umiliki wa shamba la Mlonje lililokuwa  na mgogoro kwa zaidi ya miaka 12 kati ya mwekezaji pamoja na wananchi wa Wilaya ya Sumbawanga mkoani Ruvuma.

Bunge limeazimia shauri hilo baada ya kamati maalum iliyoundwa kufuatilia mgogoro huo Mei 27 mwaka huu kuwasilisha ripoti ya uchunguzi huo bungeni Dodoma leo Agosti 27, 2024 ambapo pamoja na mambo mengine wameitaka Serikali kutaifisha shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 12,750

 “Masuala haya kwa ujumla wake yanaathiri manufaa ya shughuli za uzalishaji kwa mwekezaji na yanatofautiana na dhana ya kuwa ardhi kuwa msingi wa uhai kwa wanavijiji….

 …Kwa hiyo basi Bunge linaadhimia kwamba Serikali ibatilishe umiliki wa shamba lote la Malonje na vitalu 51 kwa maslahi ya umma,” amesema Mwenyekiti wa kamati hiyo maalumu Profesa Shukrani Manya.  

Kwa mujibu Mwenyekiti wa kamati hiyo tangu mwaka 2012 hadi  mwaka 2024 mgogoro umeibuliwa bungeni  zaidi ya mara 20 jambo lililomfanya Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson kuunda kamati hiyo iliyotakiwa kushughulikia hadidu za rejea tano ikiwemo kubaini eneo la shamba lilipoanzia na mipaka halisi ya shamba hilo pamoja na vijiji vinavyolizunguka.

Nyingine ni kubaini kama taratibu za uongezaji wa eneo zilifuatwa katika uongezaji wa eneo la shamba hilo na kama kuna vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu vinavyodaiwa kufanywa na walinzi wa shamba hilo.

Pia rejea nyingine ni kubaini iwapo vitendo hivyo vya uvunjifu wa haki za binadamu vinavyodaiwa kufanywa na walinzi wa shamba hilo, vinatokana na miongozo ya wamiliki wa shamba hilo pamoja na kubaini kama kuna jambo lolote lingine linalohusiana na mgogoro huo.

Sababu shamba la Mlonje kutaifishwa

Prof Manya amewaambia wabunge kuwa utafiti walioufanya umebaini kuwa migogoro ya shamba hilo imekuwepo tangu enzi na enzi na Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuitatua ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi kuachana na uvamizi wa mashamba hayo.

Hata hivyo jitihada hizo hazikufua dafu bado migogoro hiyo imekuwa ikiendelea kwa kipindi kirefu jambo linaloibua sintofahamu kwa wananchi wa maeneo hayo.

Pia Manya ameeleza kuwa utafiti waliofanya umebaini mwekezaji huyo kubadili matumizi ya shamba hilo kutoka matumizi ya awali ya ufugaji hadi kwenye kilimo ambapo wananchi wamekuwa wakikodi shamba hilo kwa kiasi cha Sh10,000 kwa ekari moja hadi Sh200,000 huku likiendelezwa kwa asilimia nne pekee kwa miaka 17 tangu mwekezaji huyo kumiliki shamba hilo.

Akizungumza baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya kamati hiyo, William Lukuvi Waziri wa Nchi, Bunge Sera na Utaratibu, amesema Serikali itayapitia maazimio hayo na kuyafanyia kazi.

Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inajuku,u la kuratibu shughuli zote za Serikali italifanyia kazi suala hili italiratibu vizuri sana na kuhakikisha haya yote maazimio yalioanishwa na Bunge yanatekelezwa,” amesema Lukuvi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks