Boniface Jacob afikishwa Mahakama ya Kisutu

September 19, 2024 5:24 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Afikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Meya wa zamani wa Ubungo na kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Boniface Jacob maarufu kama ‘Boni Yai’ amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Kazi Kisutu Dar es salaam leo Septemba 19,2024.

 Boni Yai amefikishwa mahakamani hapo ikiwa ni siku moja baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi jana saa kumi jioni akiwa maeneo ya Sinza.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime katika taarifa aliyoitoa jana Septemba 18, 2024 alisema jeshi hilo limemkamata na linamshikilia Jacob, mkazi wa Mbezi Msakuzi, jijini Dar es Salaam kutokana na makosa ya kijinai anayotuhumiwa nayo.

Kwa mujibu wa Wakili wa Chadema Hekima Mwasipu aliviambia vyombo vya habari kuwa polisi walimkamata Jacob na kufanya upekuzi wa takriban saa tatu nyumbani kwake.

Kukamatwa kwa Boni Yai kumezua mijadala katika mitandao ya kijamii ambapo kumekuwa na mashinikizo ya kutaka afikishwe mahakamani kusomewa mashtaka yanayomkabili kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu  (LHRC) leo kupitia mtandao  wa X zamani Twitter kimetoa wito kwa vyombo vya usalama kuhakikisha mashtaka dhidi ya Jacob yanakuwa wazi, na kwamba uchunguzi ufanywe kwa uwazi huku sheria zikizingatiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks