Rais Samia apigia chapuo matumizi ya Tehama kwa wanafunzi Tanzania

September 27, 2024 4:35 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema itawasaidia kupata majawabu na kuwaongezea uelewa wa masomo wanayosoma.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan awewataka wanafunzi wanaosoma shule zenye masomo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutumia vyema fursa hiyo kwa kujiongezea ujuzi na ufanisi katika masomo yao ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayoendelea ulimwenguni.

Hivi karibuni dunia imeshuhudia mabadiliko makubwa ya  teknolojia ikiwemo ugunduzi wa akili unde, (mnemba) inayoweza kufanya kazi kama binadamu jambo linalotarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya teknolojia kwa kurahisisha kazi na kupunguza gharama.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma leo Septemba 27, 2024 wakati wa uzinduzi wa shule ya sekondari ya wasichana iliyopewa jina lake amesema kutokana na maendeleo ya Tehama kila kitu wanachokitaji wanafunzi hao kinapatikana katika mtandao hivyo ni vyema wakajifunza na kubobea katika matumizi sahihi ya Tehama.

“Shule hii ina kitengo cha Tehama tunakokwenda dunia inahamia kwenye ICT (Information and communication technology), inahamia kwenye inaamini akili unde (artificial Intelligence) akili ambayo imeundwa na yenyewe inaunda mambo mengine,

..kwa hiyo dunia imehamia huko, na huko hatuendi tena na kalamu na karatasi, ndugu zangu itatumika ila sio kwa kiasi kikubwa lakini mambo mengi tutakuwa tunayafanya kwenye mitandao,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema wakiitumia vyema fursa ya kujifunza Tehama itawasaidia kupata majawabu ya maswali ya masomo yao kutokana na kuwa kila kitu kinapatikana katika mtandao hivyo wanatakiwa kufahamu namna sahihi ya kupata maarifa hayo.

“Nataka niwaambie siri, majawabu yote yako kwenye mitandao, yote ya wa masomo yenu, mkiingia kwenye google, mkiingia kwenye Chat Gpt, mkiingia kwenye ask all, kuna majawabu yote mnayosomeshwa hapa ndani, kwa hiyo  mkitumia vizuri mtaweza kujifunza vizuri zaidi kwa kutumia mitandao,” amesisitiza Rais Samia.

Aidha, Rais Samia pia amewataka walimu wa shule hiyo kuwalea watoto hao wa kike katika maadili mazuri ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu ya kujitambua wao ni wa kina nani na thamani yao katika jamii.

Rais Samia ametoa onyo kali kwa walimu shuleni hapo kuhakikisha wanafunzi hao hawapati ujauzito. 

 “Tusije tukasikia tena kesi hapa wangapi sijui hawakumaliza wameshikwa na ujauzito, huku msituni ujauzito unatokea wapi? utatokea wapi ukitokea walimu tutakabana shingo hapa kwa sababu huku msituni hauna pakutokea,”amesema Rais Samia. 

Hata hivyo, Rais Samia amesema Serikali yake inatambua jukumu kubwa walionalo la kukabiliana na uhaba wa maslahi pamoja na changamoto nyingine ambazo wanazifanyia kazi.

Rais Samia yupo mkoani Ruvuma kwa ziara ya siku sita ambayo inatarajiwa kuhitimishwa kesho Septemba 28, 2024 katika kilele cha tamasha la utamaduni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks