Waandishi Nukta Africa kuwania tuzo za EJAT 2023

September 19, 2024 2:50 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Esau Ng’umbi, Lucy Samson na Joshua Stephen.
  • Hii ni mara ya tano kwa waandishi wa Nukta Africa kuwania tuzo hizo.

Dar es Salaam. Waandishi wa habari watatu kutoka Kampuni ya Habari na Teknolojia ya Nukta Africa wameingia katika kinyang’anyiro cha tuzo za umahiri wa uandishi wa habari zitakazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) Septemba 28, mwaka huu.

Waandishi hao ni pamoja na Esau Ng’umbi  ambaye kwa sasa ni Mratibu wa Dawati la Habari, Lucy Patrick ambaye ni mwandishi wa habari pamoja na Joshua Stephen.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Ejat mwaka 2023  Ernest Sungura aliyekuwa akitangaza wateule hao jijini Dar es Salaam leo Alhamisi, Septemba 19,2024 amesema waandishi 72 pekee ndio wameteuliwa.

Kati ya waandishi hao wateule 25 wanaandikia magazeti, 13 mitandao ya kijamii na 20 ni kutoka redioni  huku 14 wakitokea katika runinga

“Wateule wamepatikana kwa kukidhi vigezo vya ubora ambavyo ni pamoja na ukweli, usahihi, uanuai, haki, kina, utafiti, ubunifu, uvumbuzi, upekee, uchambuzi, uwajibikaji, ufichuaji maovu, uadilifu, uwasilishaji unaoeleweka na uchunguzi,” amesema Sungura

Hii ni mara ya tano kwa Nukta Africa kuingiza washindani katika tuzo za Ejat ambapo mwaka 2022 waliingiza wateule wengi zaidi yaani wanne ambapo Daniel Samson na Suleiman Mwiru waliibuka vinara kwa kuchukua tuzo mbili kila mmoja huku Lucy Samson na Hermina Mkude wakitangazwa washindi wa tatu katika makundi wlaiyokuwa wakiwania.

Aidha, Mwaka 2021 mwandishi wa Nukta Africa Mariam John aliibuka kinara katika uandishi wa habari za madini, mafuta na gesi huku Daniel Samson akiwa mshindi wa pili wa uandishi wa habari za takwimu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa Nuzulack Dausen amesema kuteuliwa kwa wanahabari wa kampuni hiyo ni uthibitisho kuwa wanazingatia ubora wa maudhui ya mtandaoni katika kuboresha maisha ya watu.

Pamoja na kuwapongeza wanahabari walioteuliwa Dausen amewataka kutumia tuzo hizo kama chachu ya kuendelea kuzalisha maudhui yenye ubora.

“Naamini kuwa uteuzi huu utakuwa chachu kwa wanahabari wengine wa mtandaoni kufanya kilicho bora. Kama wote tukizalisha habari na makala bora tutasaidia jamii yetu kusonga mbele kimaendeleo.

“Tumefurahishwa kuona mwanafunzi wetu wa mafunzo kwa vitendo kutoka chuo kikuu Joshua Stephen naye ameteuliwa. Hii ni ushahidi tosha kuwa ubora wa maudhui ni jukumu la kila mtu na yeyote anaweza kuzalisha kilicho bora,” amesisitiza Dausen.

Nukta kufundisha waandishi, wahariri 1,000

Dausen ameongeza kuwa ili kuongeza ubora wa maudhui ya mtandaoni Nukta Africa imekusudia kufundisha wahariri na waandishi wa habari 1,000 mpaka ifikapo Disemba 2024, mafunzo ambayo pamoja na kuongeza ubora wa maudhui yatasaidia kukabiliana na wimbi la habari za uzushi ambalo limeibuka kwa kasi hasa wakati ambao nchi inajiandaa na chaguzi.

“Nukta Africa tutaendelea kutoa mafunzo kwa wanahabari kuzalisha habari bora hasa mtandaoni ili kujenga jamii yenye taarifa sahihi. 

Mwaka huu tunatarajia kufundisha wanahabari na wahariri wasiopungua 1,000 hadi Disemba na naamini mafunzo haya yatasaidia kuongeza ubora zaidi hasa kipindi hiki chenye habari lukuki za uzushi na za chini za kiwango,” amebainisha Dausen.

Mkuu wa Oparesheni na Uendeshaji wa Nukta Afrika Maphosa Banduka kwa upande wake amesema kuwania tuzo za EJAT mara tano mfululizo ni mafanikio kwa kampuni hiyo na yanadhihirisha kiwango cha juu cha weledi, bidii na ubunifu katika tasnia ya habari.

“Tunatoa shukrani zetu kwa MCT, kwani ni heshima kubwa sana kwetu kama chombo cha habari. Tuzo hizi zimeendelea kuwa kichocheo na chanzo cha motisha kwa waandishi wetu kuwa na weledi katika utoaji wa maudhui yanayosaidia jamii zetu kufanya maamuzi sahihi ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Mafanikio haya si binafsi pekee, lakini pia heshima kwa chombo chetu cha habari na kuthibitisha kwamba tuko mstari wa mbele katika kutoa maudhui bora na yenye kuleta mabadiliko kwenye jamii,” amesema Banduka.

Aidha, Joshua Stephen ambaye ni mara yake ya kwanza kuteuliwa kuwania tuzo hizo ameiambia Nukta Habari kuwa kuteuliwa katika nafasi hiyo kumempa moyo na kumfanya aongeze bidii katika utendaji wa majukumu yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks