Kada wa Chadema ‘Boni yai’ akamatwa na Jeshi la Polisi

September 18, 2024 7:56 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Jeshi la Polisi lasema linamshikilia kwa tuhuma za makosa ya jinai.
  • Lataka taarifa za kutekwa kwake zipuuzwe.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limesema linamshikilia aliyekuwa Meya wa zamani wa Ubungo, na kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Boniface Jacob ‘Boni Yai’, huku likitaka taarifa za kutekwa kwake zipuuzwe.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa kwa umma na Msemaji wa jeshi hilo David Misime leo Septemba 18, 2024 Boni Yai anashikiliwa kutokana na makosa ya jinai anayotuhumiwa nayo.

Hata hivyo, Misime katika taarifa yake amewataka Watanzania kupuuzia madai ya Boni kutekwa kama ambavyo baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wameripoti

“Jeshi la Polisi limemkamata na linamshikilia Boniface Jacob, mkazi wa Mbezi kwa Msakuzi, jijini Dar es Salaam kutokana na makosa ya kijinai anayotuhumiwa nayo.

“Hivyo, wananchi wapuuze uongo unaosambazwa mitandaoni kuwa ametekwa,” imeeleza taarifa ya Jeshi la Polisi.

Taarifa za Jacob kukamatwa, zimeanza kusambaa mitandaoni majira ya jioni leo Jumatano Septemba 18, 2024 zikieleza kuwa amekamatiwa Sinza, jijini Dar es Salaam.

Meya huyo wa zamani wa Ubungo na kada wa Chadema ni miongoni mwa wakosoaji wa masuala mbalimbali ambapo hivi karibuni ametumia mitandao yake ya kijamii kuikosoa Serikali na vyombo vya dola juu ya namna vinavyoshughulikia matukio ya utekaji na mauaji ya raia.

Kukamatwa kwa Boni Yai kunakuja ikiwa imepita siku moja tu tangu Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliagize Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua wale wote wanaohusika kupanga au kufanya matukio ya kihalifu akibainisha kuwa anazo taarifa za kiintelejensia kuwa kuna chama cha siasa kimekusudia kufanya matukio maovu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks