Rais Samia awataka Watanzania kuungana kukemea mauaji

September 17, 2024 7:20 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema damu ya kila Mtanzania ina thamani bila kujali itikadi, kabila au rangi.
  • Asikitishwa na ukimya wa watu kwenye baadhi ya matukio ikiwemo mauaji ya walemavu wa ngozi na wazee.
  • Azionya jumuiya za kimataifa kutoiamuru Tanzania jambo la kufanya kuhusu kulinda uhai wa wananchi wake.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuungana na kukemea vitendo vya mauaji vinavyotokea nchini ili kukomesha matukio hayo badala ya kutoa shutuma na matusi kwa Serikali huku wakiacha jukumu la kudhibiti uhalifu kwa vyombo vya dola pekee.

Hivi karibuni kumeripotiwa matukio ya utekaji na mauaji ambapo baadhi ya wananchi wamenyooshea vidole vyombo vya dola kushiriki katika matukio hayo ikiwemo mauaji ya aliyekuwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyeuawa baada ya kutekwa kwenye basi la Tashrif akiwa safarini kuelekea mkoani Tanga.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Polisi Tanzania ameungana na Watanzania pamoja na jumuiya za kimataifa kulaani tukio hilo akiongeza kuwa uhai wa Mtanzania yoyote unathamani sawa bila kujali itikadi, kabila, rangi au umajumui wake hivyo linapotokea tukio lolote umma unatakiwa kuungana kukemea na si kwa baadhi ya watu pekee.

“Kifo cha ndugu yetu Kibao kimeibua wimbi kubwa, kulaani, kusikitika, kulaumu, kuita Serikali ya wauaji, hii sio sawa, kifo ni kifo, tunachotakiwa kufanya Watanzania wote tukemeane, tusimame imara kukemea mambo haya, damu ya Mtanzania ituume, tusiwe tunamwaga damu bila sababu,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameelezea masikitiko yake juu ya mauaji ya watu wenye ualbino, wazee, watoto, na wanafamilia akitaja matukio hayo kama ishara ya baadhi ya wanajamii kupoteza utu na kuongezeka kwa uhalifu mkubwa, ambapo hata watu mashuhuri na viongozi wa dini wamehusishwa hali inayowakatisha tamaa wananchi.

Kwa mujibu wa Rais, ili kukomesha mwenendo wa kujirudia kwa matukio ya mauaji, wananchi wanapaswa kutoa taarifa za matukio hayo ikiwemo ya kikatili pindi yanapotokea kwa kuwa matendo hayo hufanyika miongoni mwa wanajamii wenyewe, akisisitiza pia umuhimu wa polisi kuwa karibu zaidi na jamii ili kufuatilia matukio hayo.

“Lakini yanapotokea haya yanatokea kwenye maeneo yetu huko tunakaa kimya mpaka polisi iibuke iseme wengine hawasemi…inasikitisha kuona mambo haya ya mauaji yanatokea katika maeneo tunayoishi, inawezekana wananchi tunayaona lakini hatutoi taarifa na hapa ndio kunakuja ule umuhimu wa polisi kuweko kule kwa jamii katika kata husika ili kuweza kuyafuatilia kwa karibu zaidi,” amesema Rais Samia.

Hatutaelekezwa cha kufanya

Hata hivyo, Rais Samia ametumia nafasi hiyo ya kuhitimisha mkutano wa maafisa waandamizi wa Jeshi la Polisi 2024 kuonya wawakilishi wa jumuiya za kimataifa ambao wamekuwa wakitoa maelekezo ya nini Serikali ya Tanzania inapaswa kufanya ili kukabiliana na matukio ya mauaji na utekaji yanayoendelea kuripotiwa.

Rais Samia ameeleza kuwa Tanzania inaongozwa na katiba yake, ambayo inatoa maelekezo ya jinsi ya kuendesha Serikali na kulinda maslahi ya Watanzania hivyo hakuna haja ya kupokea maelekezo kutoka nje kuhusu jinsi ya kutekeleza majukumu yao ya kikatiba.

“Tumeapa kuilinda na kuitetea katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba tutafanya kila linalowezekana kuimarisha ulinzi wa maisha na uhai wa Watanzania kwa kuwa ni jukumu letu, kwenye wajibu huu wala hatuhitaji kuelekezwa na mtu yeyote nini cha kufanya kwasababu katiba yetu inamaelekezo yote jinsi ya kuendesha Serikali yetu na hakuna mtu anaeumia haya yanapotokea kama tunavyoumia Watanzania,” amesema Rais Samia kwa msisitizo.

Aidha, Rais Samia  amebainisha kuwa ni umuhimu kufuata makubaliano ya kimataifa kama yalivyoainishwa katika Mkataba wa Vienna kuhusu Mahusiano ya Kidiplomasia ya mwaka 1961, ambao unasisitiza kuheshimu uhuru wa kila nchi na kufuata kanuni za mahusiano ya kidiplomasia. 

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza katika maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Polisi Tanzania na kufunga mkutano wa maafisa waandamizi wa jeshi hilo. Picha. Ikulu

Angalizo kwa Jeshi la Polisi

Ili kuongeza imani ya Jeshi la Polisi kwa Wananchi Rais Samia amelitaka jeshi hilo udumisha maadili na uwajibikaji katika utendaji wao wa kazi kwa kuzingatia dhima yake ya ulinzi wa raia na mali zao na kusimamia sheria.

Kwa mujibu wa ripoti za Haki ya Binadamu kutoka Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kutoka 2016 hadi 2023 jumla ya matukio 50 ya mauaji ya raia yamesababishwa na matumizi ya nguvu kupita kiasi na ukatili wa maafisa wa vyombo vya dola hususan wa Jeshi la  Polisi na Jeshi Usu.

Ripoti hiyo imeeleza pia ndani ya mwaka mmoja matukio ya ukamataji na uzuiwaji kinyume na sheria yameongezeka kwa asilimia 325 kutoka matukio 12, 2022 hadi matukio 51, 2023, walengwa kwa kiasi kikubwa wakiwa ni Waandishi wa Habari na Wanasiasa wa vyama pinzani.

“Kama walinzi wa raia na mali zao, Jeshi la Polisi ndio wasimamizi wa haki na sheria hivyo halipaswi kuhusishwa au kuhisiwa na ukiukwaji wa sheria na haki inazozisimamia…hivyo nendeni kusimamia maadili ya askari ili jeshi litoe huduma stahiki na kuongeza imani ya wananchi kwa chombo chao hiki,” ameelekeza Rais Samia.

Historia ya Jeshi la Polisi

Jeshi la Polisi Tanzania lilianzishwa rasmi tarehe 25 Agosti 1919, kwa tangazo la Serikali ya Kiingereza lililotolewa katika Gazeti la Serikali, Vol.1 No.21-2583, wakati huo likijulikana kama Jeshi la Polisi Tanganyika likiundwa na wanaume pekee. 

Makao makuu ya kwanza ya jeshi hilo yalikuwa Wilayani Lushoto, Mkoani Tanga chini ya uongozi wa Major S.T Davis, huku Elangwa Msangi akiwa Inspekta Jenerali wa kwanza baada ya cheo hicho kuanzishwa Julai 1, 1964.

Wakati jeshi hilo likiadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake huenda likakabiliana na wakati mgumu wa kurejesha imani kwa wananchi kutokana na ushiriki wa baadhi ya watumishi wachache katika vitendo vya uhalifu jambo linalotia doa utendaji kazi wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks