Utalii wa Kasa Zanzibar kutoa ajira kwa vijana

August 24, 2024 3:16 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Rais Samia asema kupitia mradi huo vijana wazawa wataweza kumudu gharama za maisha.

Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan amesema mradi mpya wa utalii wa samaki aina ya kasa uliopo katika mapango ya Salam visiwani Zanzibar utachochea upatikaji wa fursa ajira kwa vijana wazawa wanaoishi maeneo hayo.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mapango hayo visiwani Zanzibar leo Agosti 24, 2024 amesema kuwa mradi huo utawewezesha vijana wa eneo hilo kukuza vipato vyao na kumudu gharama za maisha.

“Kuweka mradi huu hapa kumetengeneza ajira kwa vijana…kuwatengenezea vijana maslahi yao ya kiuchumi na kuwahakikishia wanaishi vizuri, wanakwenda hospitali vizuri, haja zao wanazipata vizuri kwa sababu fedha inaingia mkononi,” amesema Rais Samia.

Huenda kuongezeka kwa ajira kutoka sekta binafsi kukapunguza wimbi la utegemezi wa kifedha kwa mtu mmoja mmoja nchini ambao ripoti mpya ya Fincope inautaja kuongezeka kwa asilimia tano ndani ya miaka sita.

Ripoti hiyo iliyotolewa Julai 10, 2023 na Mfuko wa Kuendeleza Huduma za Fedha Tanzania (FSDT) inasema mwaka 2017 Tanzania ilikuwa na asilimia 18 za utegemezi kifedha zilizoongezeka hadi kufikia asilimia 23 mwaka 2023.

Rais Samia Suluhu Hassan akishuhudia utalii wa Kasa katika Pango la Salaam, Kizimkazi visiwani Zanzibar.Picha|Ikulu.

Mapango ya Salaam kutunza mazingira

Mbali na mapango hao kuchochea upatikanaji wa fursa za ajira kwa wazawa, Waziri wa Nchi, Muungano na Mazingira Dk Ashatu Kijaji amesema mradi huo utasaidia kutunza mazingira.

“Sio kwa ajili ya utalii tu lakini hii inakwenda kuwa motisha kwenye utunzaji wa mazingira yetu kwa sababu mazingira ni fedha na mazingira ndio yanayotufanya tuwe salama…

…Tunakuahidi kuendelea kutunza mazingira ili tuweze kutengeneza vivutio vingi vya utalii lakini maeneo mbalimbali ya kutengeneza fedha na kujenga uchumi wa watanzania,” amesema Dk Kijaji.

Utunzaji wa mazingira katika eneo la mapango ya Salaam visiwani Zanzibar umetengeneza makazi ya samaki aina ya kasa wanaofanya mamia ya watalii kutembelea visiwa hivyo.

Miongoni mwa utalii unaofanyika katika kivutio hicho ni kupiga picha, kuogelea na kulisha samaki hao aina ya kasa.

Katika hatua nyingine Rais Samia ameagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuingiza kivutio hicho katika orodha ya vivutio vya utalii nchini ili kuendelea kukitangaza kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks