KANUNI YA 4: Kwanini unatakiwa kupumzika baada ya kazi?

Joshua Sultan 0243Hrs   Januari 18, 2020 Kolamu
  • Kumpuzika kunasaidia kuimarisha misuli ya mwili, ufanisi wa utendaji na kazi.
  • Pia ni sehemu ya kukabiliana na msongo wa mawazo na sonona.
  • Usipojenga tabia ya kumpumzika matokeo yake ni kuongeza uwezekano wa magonjwa kama shinikizo la juu la damu.

Fanya kazi kama mtumwa ili baadaye uishi kama mfalme ndiyo msemo iliozoeleka kila siku kwa watu. Ndiyo hatuna budi kufanya kazi ili tupate riziki ya kila siku na kupata maendeleo tuliyokusudia. Lakini vipi kuhusu kupumzika? 

Miili yetu inafanya kazi kila wakati kwa kila kiungo. Hata moyo ambao hupiga maisha yako yote mpaka siku uhai utakapokoma hupumzika kati ya pigo moja na lingine. 

Hata kama tunashauri kufanya mazoezi na kadhalika lakini mpango wa mazoezi haupo kamili bila kuwa na mapaumziko kila siku. 

Kwa msingi huo utapata majibu kuwa ni kwanini mgonjwa anapoletwa hospitali kitu cha kwanza ni kupewa kitanda alazwe. Hii ni kwa sababu mwili unahitaji kupumzika ili sasa uweze kujihami na kurejea katika usawa. 

Mifumo  mingine ipumzike ili mifumo ya ulinzi ifanye kazi kwa ufanisi bila  kuingiliana. Kwa lugha ya simu ama kompyuta za kisasa tunaweza sema ya kuwa mwili unahitaji kupumzika ili uji-“reboot” (kujihuisha).


Kwanini kumpumzika ni muhimu 

Kupumzika sio uzembe. Bali kupumzika pasi na kufanya kazi yaani kupita kiasi ndiyo uvivu na uzembe. Baada ya majukumu ya uzalishaji mali ni muhimu mwili upumzike. 

Kupumzika ni muhimu ili kuifanya misuli iimarike na ikue. Kwa mfano unavyofanya mazoezi, hufanya misuli ichanike michano midogo midogo, lakini unapopumzika seli ziitwazo “fibroblasts” hurekebisha vijidonda hivi.


Huongeza ufanisi na utendaji wako wa kazi

Ni vyema kupata mapumziko baada ya kazi na kuwa na tabia ya kupumzika kila baada ya majukumu. Huongeza ufanisi, kimsingi ubongo wako hupata nafasi ya kupumzika na kuufanya mwili kuwa angavu na kuondosha uchovu. 



Zinazohusiana:



Huondosha mkazo na sonona

 Changamoto nyingi zinazoweza kukupata huweza kukufanya uone hauna  haja ya kupumzika. Lakini ukikaa ukatulia na glasi ya maji na kupata hewa safi, hufanya mzunguko wa damu uongezeke. 

Hii hurutubisha ubongo wako na seli zingine za mwili. Inakufanya kuondosha msongo na kutafakari kwa ubora wa hali ya juu. Pia husaidia kuondosha uchovu ambao kwa kiasi kikubwa huchangia kupata sonona na mkazo.

Hata kama tunashauri kufanya mazoezi na kadhalika lakini mpango wa mazoezi haupo kamili bila kuwa na mapaumziko kila siku. Picha|Medical News Today.


Huchangia kuwa na usingizi mzuri 

Kufanya kazi na mazoezi hufanya mwili utengeneze homoni ambazo hufanya kuongezeka kwa nguvu ya mwili kama “adrenaline na cortisol”, lakini homoni hizi usipopumzika huzidi kiwango na kukufanya kupata shida wakati wa kulala.

Pia kupumzika huusisha kupata usingizi mapema hasa wa usiku. Lala mapema kwa utulivu kisha amka ukiwa na akili mpya na ufanisi.

Ni muhimu kutambua ya kuwa kufanya kazi kwa bidii ni muhimu. Lakini pia mwili unahitajji mapumziko ili kuongeza ufanisi wa utendaji wako. Hakuna maana kujinyima mapumziko. 

Usipojenga tabia ya kumpumzika matokeo yake ni kuongeza uwezekano wa magonjwa kama shinikizo la juu la damu, matatizo ya kisaikolojia kama mkazo. Hatari ya kiharusi na kushindwa kujihusisha na jamii. Uchovu uliopitiliza na hata upungufu wa uwezo wa utendaji wa ubongo.

Dk Joshua Lameck Sultan ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba katika Chuo cha Tiba na Sayansi Shirikishi Moshi (KCMC) pamoja na hospitali ya KCMC. Pia ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) ambapo hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.

Related Post