Ajira sekta binafsi, serikalini zapungua

Daniel Samson 0905Hrs   Agosti 10, 2019 Habari
  • Ajira rasmi zilizotengenezwa na sekta binafsi zimepungua kutoka 239,017 mwaka 2016/2017 hadi kufikia ajira 137,054 mwaka 2017/2018.
  • Pia ajira rasmi zilizotengenezwa na Serikali zilipungua kutoa 82,302 hadi 18,000 ikiwa ni sawa na anguko la asilimia 78.1 katika kipindi hicho cha mwaka mmoja.

Dar es Salaam. Ripoti mpya ya takwimu za Tanzania imeeleza kuwa ajira zinazotengenezwa na sekta binafsi zimepungua kwa asilimia 42.6 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita, jambo linalotoa changamoto kwa vijana na wadau wa maendeleo kubuni njia mbadala za kuondoa tatizo la ajira nchini. 

Ripoti hiyo iliyopewa jina la “Tanzania in Figure 2018” iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Juni 2019, inaonyesha kuwa ajira rasmi zilizotengenezwa na sekta binafsi zimepungua kutoka 239,017 mwaka 2016/2017 hadi kufikia ajira 137,054 mwaka 2017/2018. 

Hiyo ni sawa na anguko la asimilia 42.6 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja katika sekta hiyo inayotegemewa kuajiri watu wengi nchini. 


Zinazohusiana: 


Hali hiyo inaweza kuwa imesababishwa na na kupungua kwa shughuli za biashara katika kipindi ambazo zilikuwa zinakabiliwa mazingira yasiyoridhisha kwa wawekezaji ikiwemo urasimu katika upatikanaji wa vibali na utitiri wa kodi na tozo.

Hata hivyo, katika bajeti ya mwaka 2019/2020, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali imekusudia kuboresha mazingira ya biashara kwa kuondoa kodi na tozo zinazowaumiza wawekezaji. 

Pia ajira rasmi zilizotengenezwa na Serikali nazo zilipungua kutoa 82,302 hadi 18,000 ikiwa ni sawa na anguko la asilimia 78.1 katika kipindi hicho cha mwaka mmoja. 


Wakati ajira rasmi serikalini na sekta binafsi zikipungua, ajira zilizotokana na miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ikiwemo ujenzi wa barabara, majengo na reli ziliongezeka na kuifanya sekta hiyo kuongoza kwa kuajiri watu wengi zaidi mwaka mmoja uliopita. 

Licha ya kuongezeka kwa mahitaji ya ajira Tanzania, kiwango cha watu wasio na ajira kimeendelea kupungua katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. 

Mathalani, kiwango hicho cha ukosefu wa ajira nchini kimepungua kutoka asilimia 10.3 mwaka 2014 hadi asilimia 9.7 mwaka 2018. 

Related Post