'Sheria Kiganjani' kimbilio kwa wanaosaka haki mtandaoni

Zahara Tunda 0202Hrs   Februari 12, 2019 Teknolojia
  • Inawasadia wa wananchi kupata uelewa wa sheria na kutatua migogoro midogo midogo kwa urahisi.
  • Ni programu ya simu (App) inayosaidia kupunguza pengo la upungufu wa watoa huduma za ushauri wa kisheria kwa sababu wananchi wengi watapata huduma hii popote walipo kwa wakati mmoja.
  • Ni jukwaa muhimu linalowakutanisha wananchi na Mawakili katika maeneo mbalimbali nchini.

Dar es Salaam. Huenda changamoto ya kutokujua sheria kwa wananchi ikapungua nchini, baada wabunifu kuja na programu tumishi (App) inayowasaidia kupata tafsiri na elimu ya sheria, kukutana na mawakili waliobobea kuwawakilisha katika kesi zao mahakamani. 

Juhudi hizo ni mkakati wa wadau kuhakikisha teknolojia inakuwa sehemu ya kurahisisha maisha na kuwawezesha wananchi kupata haki zao katika viganja vyao. 

App hiyo inayotambulika kama Sheria Kiganjani  imetengenezwa na vijana wa kitanzania wakiwa na nia ya kuziba pengo la upungufu wa watoa huduma za ushauri wa kisheria kwa sababu wananchi wengi hawapati huduma hizo katika maeneo waliyopo. 

Sheria Kiganjani iliyoanzishwa Agosti 2018, inamsaidia mwananchi kupunguza gharama za kupata msaada wa kisheria na kuhakikisha inaziba pengo la uhaba wa wanasheria katika nchi yetu ili haki na wajibu wa kila mwanajamii kujua sheria utekelezwe kivitendo.

"Sheria Kiganjani wameamua kwa dhati kuanzisha mfumo huu wa upatikanaji wa huduma za kisheria kwa njia ya mtandao, ambayo itashusha gharama za huduma ya sheria kwa zaidi ya 80% (asilimia themanini) ukilinganisha na gharama za sasa," inaeleza sehemu ya taarifa ya App hiyo. 

Mpaka sasa App hiyo iliyofanikiwa kuwafikia watu 4,000 imepokea malalamiko zaidi ya 1,500 kutoka kwa watu mbalimbali ambapo mtumiaji anaweza kutumia njia ya kupiga simu, kutuma ujumbe mfupi wa maneno (SMS) au ujumbe wa mtandaoni kupata huduma za kisheria.

Malalamiko yanayowasilishwa zaidi ni kesi za ndoa, mirathi na ardhi hasa kutoka mikoa ya kanda ya ziwa, jambo linalowapa fursa ya kuendelea kufanya tafiti zaidi ili kuwasaidia wananchi wenye changamoto hizo.  


Timu ya vijana wanaoiwezesha App ya Sheria Kiganjani  kuwafikia watu wengi wanaohitaji msaada wa kisheria. Picha|Nabiry Jumanne.

Kinachoipa nguvu App hiyo ni matumizi ya lugha ya Kiswahili ambayo inazungumzwa na watu wengi nchini, jambo linaloondoa changamoto ya watu kutokuelewa lugha ya kitaalamu inayotumiwa katika maandiko ya kisheria.

Ripoti ya utafiti wa masuala ya kifedha ya Finscope ya mwaka 2017 inabainisha kuwa watu saba kati 10 (asilimia 72) nchini wanaweza kusoma na kuandika Kiswahili vyema ikilinganishwa na takriban watatu tu kwa kila 10 wanaoweza kufanya hivyo katika Kiingereza.

“Upekee wa Sheria Kiganjani ni kupata elimu na nyaraka za kisheria pamoja na kuongea moja kwa moja na mawakili juu ya ushauri kwa simu yako ” anasema Meneja Miradi wa Sheria KIganjani, Nabiry Jumanne.

Ufanisi na utendaji wa Sheria Kiganjani uliiwezesha kupata tuzo ya Apps bora katika mashindano ya Innovation Express Dar es Salaam inayotolewa na kampuni ya Mastercad kwa kushirikiana na Taasisi ya ukuzaji sekta ya Fedha Tanzania (FSDT) Novemba, 2018.

Kutokana na ukweli kuwa App hiyo imekuwa msaada kwa watu wengi, watumiaji wake wanatakiwa kuchangia kiasi cha Sh2,000 tu kwa mwezi ili kupata huduma hiyo na kusaidia katika uendeshaji wa shughuli za kiofisi.


Zinazohusiana: NALA yaja na teknolojia ya kijanja kutuma, kupokea pesa

                           Startups za Tanzania zilizotamba mwaka 2018


Hata hivyo, waanzilishi wa Sheria Kiganjani wameiomba Serikali iangalie namna ya kupunguza kodi inayotozwa kwa kampuni zinazochipukia ili kuziongezea nguvu ya kukua na kuimarika.

“Serikali pia iangalie namna itakavyopunguza makato hasa kwa kampuni changa za wabunifu wa teknolojia, ili tuweze kuisaidia jamii,” amesema Jumanne.


Wadau wa sheria waipa tano

Wadau wa masuala ya sheria wanaona ujio wa App ya Sheria Kiganjani  ni fursa kwa mawakili ambao hawana ajira kuunganisha nguvu na kujisajili ili waweze kuwafikia wateja katika maeneo mbalimbali nchini.

“Nimewahi kuisikia lakini sijawahi kuitumia ila inaweza kuwa fursa kwa mawakili,” amesema Wakili wa Kujitegemea, Benedict Temba.

Pamoja na hayo Afisa Programu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti ameiambia Nukta kuwa uwepo wa App hiyo utaongeza wigo wa upatikanaji wa haki hasa katika maeneo yenye changamoto ya uhaba wa mawakili na mahakimu.

Related Post